Michezo

NINAONEWA: Bure bilashi ninaonewa miye, alia Ozil

October 18th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MESUT Ozil amelalamikia hatua ya kutumiwa kama ‘kisingizio’ kila mara Arsenal inapopoteza mechi kubwa.

Kiungo huyo, ambaye hupokea mshahara wa Sh46.4 milioni kila wiki katika kandarasi yake uwanjani Emirates, ametengwa kabisa na kocha Unai Emery, na amefanikiwa kushiriki mechi mbili pekee msimu huu.

Ozil, ambaye ameanza mechi moja pekee ligini msimu huu, ana wakosoaji wengi, lakini amejitetea katika mahojiano na gazeti la The Athletic kuwa anaamini madai anayoelekezewa ni uonevu.

“Tunapokosa kufanya vyema katika mechi kubwa, inasemekana mimi ndiye chanzo. Ikiwa ni kweli wanavyodai, basi utaelezea vipi kuhusu matokeo yetu katika mechi kubwa ambazo sijashirikishwa? Sijaona kama kuna utofauti katika matokeo,” aliambia The Athletic.

“Najua watu wanatarajia nitoe mchango mkubwa, niendeshe shughuli na kuleta utofauti kwenye mechi, na ninafanya hivyo, pia, lakini si kitu rahisi.

“Mimi si timu ya mtu mmoja, kuna wachezaji wengine pia, na usisahau kuwa baadhi ya wapinzani wetu ni bora kutuliko.”

Emery amepoteza imani na Ozil. Msimu uliopita, Mjerumani huyu aliachwa nje ya mechi kadha za ugenini na haijakuwa tofauti sana na msimu huu ambapo amekosa mechi tatu zilizopita za ligi.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 31 ameachwa nje ya kikosi kabisa katika mechi hizo tatu zilizokuwa kwenye mashindano yote ambazo ni dhidi ya Manchester United uwanjani Old Trafford na Standard Liege na Bournemouth uwanjani Emirates.

“Nilipoamua kutomjumuisha Ozil kikosini nilikuwa na sababu. Niliona kuna wachezaji wengine waliostahili nafasi hiyo zaidi,” Emery alisema baada ya Arsenal kulipua Standard Liege 4-0 mnamo Oktoba 3 kwenye soka ya Ligi ya Uropa.

Ozil alilazimika kukosa mwanzo wa msimu baada ya yeye pamoja na mchezaji mwenza Sead Kolasinac kushambuliwa na watu waliokuwa wakiendesha pikipiki kaskazini magharibi mwa London na kisha kutokana na “visa zaidi vya kiusalama”.

Hata hivyo, kiungo huyo amegharimu Arsenal Sh2.6 milioni kila dakika na kuichezea dakika 142.

Kandarasi ya sasa ya Ozil itakatika miaka miwili ijayo na licha ya kukosa kuchezeshwa, amesisitiza kuwa atahakikisha ameimalizia uwanjani Emirates.

“Niko na kandarasi hapa hadi katikati ya mwaka 2021. Kabla ya siku hiyo kufika, mimi bado niko hapa,” alisema.

“Unaweza kupitia magumu, kama haya, lakini hiyo si sababu ya kutorokea kwingine na sitafanya hivyo. Niko hapa angaa hadi mwaka 2021.”

Mapema Oktoba kiungo wa zamani wa Arsenal, Ray Parlour aliambia tovuti ya talkSPORT, “Ozil sasa hata hayuko kikosini. Nadhani pengine wakati wake katika klabu ya Arsenal umefikia ukingoni. Kuna machipukizi ambao wanastahili fursa hiyo pengine zaidi kumliko wakati huu.”

Arsenal haina mechi hadi Jumatatu itakapozuru Sheffield United.

Vijana wa Emery wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 15 nao Sheffield wako katika nafasi ya 13 kwa alama tisa.

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp inaongoza ligi hii kwa alama 24 baada ya kushinda mechi zake nane. Iko alama nane mbele ya Manchester City ya kocha Pep Guardiola. City ndio mabingwa watetezi.