Ninapolewa na kuvuta bangi, ajuza wote hugeuka vipusa, shabiki wa Chelsea aambia mahakama

Ninapolewa na kuvuta bangi, ajuza wote hugeuka vipusa, shabiki wa Chelsea aambia mahakama

Na Richard Munguti

KONDAKTA mwenye umri wa miaka 27 Jumanne aliwavunja watu mbavu mahakamani alipoungama kuwa akilewa pombe aliyoiita Blue Ice huwaona kina mama wa umri wa miaka 70 na zaidi wamegeuka kuwa vidosho na vipusa “na wananisisimua sana.”

“Ukweli wa mambo mheshimiwa ni kwamba pindi ninapomimina Blue Ice moja tu kisha nipige pafu kadhaa za bangi na sigara ya Safari nawatazama kina mama wote wenye umri wa miaka 70 na zaidi na wanageuka vipusa wa miaka 16 hadi 28. Ni watamu wacha tu,” Wyclife Alloys Orinda alimweleza hakimu mkuu Bi Martha Mutuku.

“Eti umesema nini?” Hakimu Bi Mutuku alimwuliza Orinda aliyeshtakiwa kwa kuzua fujo na kuhatarisha maisha ya watu katika jengo la Revlon Plaza Biashara Street mnamo Januari 11,2021.

Orinda alikiri alimtusi Mary Nyaguthii na kuburuta kibandiko cha tangazo katika duka lake.

Akijibu hakimu, Orinda alisema: “Mheshimiwa nimekueleza mimi nawachangamkia kina mama wazee ninapolewa pombe aina ya Blue Ice, Seneta nikiendelea kuvuta sigara aina ya Safari na kuchanganya na pafu kadha za Bhangi. Sigara hiyo ya Safari inanifanya kuona niko safarini kwenda nchi ya Kanaani tunakoahidiwa na Baba, Raila Odinga.”

Makanga huyo anayehudumu na matatu za barabara ya nambari 8 zinazobeba abiria kati ya Kibera na Westlands alisema Blue Ice inamfanya kutazama kwa makini timu ya kandanda ya Ulaya ya Chelsea inayovaa jezi za samawati.

“Hiyo timu ya Blue ndiyo timu ninayoshabikia sana. Bangi inanifanya kufanyakazi kwa bidii mpaka ninapeleka pesa kwa Benki ya Co-operative,” alisema Orinda.

Aliishangaza mahakama alipoungama kuwa mlalamishi (Mary Nyanguthii) “anayedai nilimtukana ni binamu ya mke wangu Carolyne Wangui Kinyanjui mwenywe umri wa miaka 45 na mimi niko na umri wa miaka 27.”

Alisema Carolyne ameajiriwa na Mary na siku ya Januari 11 alipokuwa ameenda kumsihi amruhusu kuona watoto wao wenye umri wa miaka mitatu na miezi 9 mtawalia.

“Nilizua vurumai waliponikataza nikiona watoto wangu na kucheza nao. Waliita polisi kunikamata. Mimi sio mwenda wazimu eti niwatese watoto wangu na mke wangu anayenizidi na umri,” alisema

Aliendelea kudai kuwa walikutana na Carolyne kama analewa pombe na kuvuta sigara pamoja na bhangi.

“Kila ninapolewa ninapata maarifa ya kuwabembeleza kina mama hawa wa umri mkubwa kuliko mimi. Nilimshawishi Carolyne akanikubali. Nilikuwa mlevi barabara nilipomchumbia Carolyne hata akanipenda na nikamzalia watoto wawili wazuri sana,” alisema mshtakiwa.

Alimweleza hakimu kwamba mwaka uliopita kina mama hao walimsingizia amezua vurugu ndipo akafungwa jela na alipokamilisha kifungo alipata Carolyne na watoto wamehama Eastleigh walipokuwa wakiishi.

Walienda kuishi Mwimto. Aliomba mahakama iamuru akubaliwe kuwaona watoto wake.

“Je, kama uko mlevi jinsi hii unafikiria hii korti inaweza kukubalia uwaone watoto hao. Si utawadhuru?” Bi Mutuku alimwuliza. “Hapana, hao ni watoto wangu siwezi kuwadhuru kwa njia yoyote ile,” mshtakiwa alimjibu.

Bi Mutuku alimweleza Orinda kwamba atazuiliwa ndipo ahojiwe na maafisa wa urekebishaji tabia ibainike tabia yake. Mshtakiwa atarudishwa tena kortini Januari 28, 2021 hatima yake iamuliwe

You can share this post!

Olunga ayoyomea Qatar ‘kumumunya mamilioni’

MARY WANGARI: Elimu kuhusu afya ya uzazi itiliwe maanani...