Habari Mseto

'Ninashona barakoa moja kwa dakika 15'

April 17th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Barakoa zimeokoa biashara ya fundi cherehani Jacob Onyango ambayo ilikuwa inazama kutokana na uhaba wa wateja kwa sababu ya janga la virusi hatari vya corona.

Onyango ana duka la kushona nguo mtaani Kariobangi South Civil Servants katika kaunti ya Nairobi. Kwa miaka 15, amekuwa akishona suti. Hata hivyo, alilazimika kujifunza kutengeneza barakoa baada ya janga lilo hilo kumfungulia mlango mwingine.

“Biashara yetu hapa huwa ni kushonea wateja suti. Tulikuwa tunauza angaa suti tatu kila wiki kabla ya janga la virusi vya corona. Hata hivyo, hatujaona mteja hata mmoja amekuja hapa kwa kipindi cha mwezi mmoja na wiki moja hivi kupima suti. Tulikuwa tunauza kila suti Sh4,500,” alieleza Onyango, ambaye ni mmiliki wa duka hilo na ameajiri watu wengine wawili.

“Badala ya kukaa tu tukijisikitia kwa sababu biashara ilikuwa imeenda chini sana, tuliamua kushona barakoa. Barakoa sasa inafanya mwisho wa siku tuende nyumbani na chakula. Tulianza kushona barakoa Aprili 1. Kila mmoja wetu anashona barakoa 20 kila siku. Kutoka barakoa 60 tunazoshona, robo tatu huwa zinanunuliwa kila siku. Tunauza barakoa moja Sh50,” anasema Onyango.

Bernard Wanjare, ambaye ni mmoja wa watu wanaofanya kazi na Onyango, anasema hawakuwa na ujuzi wa kushona barakoa. “Tulitumia mtandao wa YouTube kupata mafunzo ya kushona barakoa. Ujuzi huo tulipata kutoka kwa Mjerumani mmoja, ambaye alikuwa anapeana mafunzo hayo. Ilinichukua binafsi dakika 10 kupata maarifa hayo kwa sababu kazi yetu ni ya fundi wa nguo,” alisema Wanjera, huku akionyesha mwandishi huyu jinsi wanavyotengeneza barakoa.

Anasema walifikia uamuzi wa kuuza barakoa Sh50 kwa sababu ya mali ghafi wanayotumia na pia uwezo wa wananchi kununua.

Onyango anasema kuwa bei ya barakoa katika duka lake ni moja tu iwe mtu mzima ama mtoto kwa sababu mbinu ya kuzitengeneza na nyenzo ni zile zile.

“Tunashona barakoa moja kwa kati ya dakika 15 na 25 kwa kutegemea kama tunaweka mipira ya kunyumbulika ama kamba ya kushonwa. Barakoa za kamba zinachukua muda mwingi,” anasema Onyango na kufichua kuwa kuna wateja wanaopenda barakoa zilizoongezwa nyumbufu kwa sababu ni rahisi kuvaa. “Wengine hawapendi barakoa za nyumbufu kwa sababu wanasema zinawaumiza masikio,” Onyango alieleza Taifa Leo katika mahojiano.

Kuhusu rangi ya barakoa ambazo Wakenya wananua sana, Onyango anasema, “Watu wanapenda sana rangi nyeupe na buluu, ingawa kila mtu huwa na rangi anayopenda zaidi kuliko zingine.”

Hata hivyo, anasema watu wengi wanaona aibu kuvalia barakoa. Pia, kuna wale walio na dhana kuwa wakivalia buluu wataonekana kama wahudumu wa afya kwa hivyo wanachagua barakoa za rangi hiyo. “Kama si faini kali (Sh20,000) ama kufungwa jela miezi sita, sidhani kama watu wengi wangevalia barakoa. Wengi wanazivalia kwa sababu wamelazimishwa,” anasema.

Onyango alikamilisha mahojiano haya kwa kushauri Wakenya, “Kila mtu ajilinde. Osha mikono inavyotakikana. Dumisha usafi. Tufuate maagizo na tutakuwa salama. Tujilinde.”