Ninauza mayai ya Sh1.5m kila siku – Ruto

Ninauza mayai ya Sh1.5m kila siku – Ruto

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amefichua kuwa yeye huingiza Sh1.5 milioni kila siku kutokana na mauzo ya mayai 150, 000 kutoka biashara yake ya ufugaji kuku katika kaunti ya Uasin Gishu.

Akiongea Alhamisi katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi, Dkt Ruto alisema hayo ndiyo maelezo ambayo Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i alikosa kutoa alipowasomea wabunge orodha ya baadhi ya mali yake yaliyoko sehemu mbalimbali nchini.

“Wangeongeza kwamba katika biashara yangu ya kuku, nina kuku 200,000 ambao hunipa mayai 150,000 kila siku ambayo huniingizia Sh1.5 milioni kila siku,” akasema.

Dkt Ruto ambaye alikutana na ujumbe wa wanasiasa kutoka kaunti ya Nakuru, alisema kuwa orodha ya mali ambayo Dkt Matiang’i aliwasilisha bungeni haikuwa kamilifu kwani haikujumuisha mali yake yote.

“Vile vile, hao watu wa OP (Afisi ya Rais) hawakufanya kazi kamilifu. Hata walikosa kusema kuwa niko na hisa 400,000 katika Safaricom na zingine 40,000 katika Kenya Airways,” akaeleza.

Dkt Ruto alisema orodha hiyo iliwasilishwa na Dkt Matiang’i mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Usalama Jumatano, iliyumuisha mali zingine ambazo sio zake.

“Kwa mfano hiyo shamba ya ADC Mutara ya ukubwa wa ekari 15,000 iliyoko Laikipia sio yangu. Hapo nitamwambia Matiang’i afanye marekebisho kidogo,” akawaambia wajumbe hao walioongozwa na Seneta wa Nakuru Susan Kihika na Mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki David Gikaria.

Dkt Matiang’i alisema Waziri Matiang’i alifanya kazi nzuri kuliko vyombo vya habari ambavyo vilidai anamiliki mali kadhaa ambazo sio zake.

“Katika ukaguzi wao haramu, vyombo vya habari vilidai ninamiliki hoteli ya Six-Eighty na Boulevard ambayo haiku kwenye orodha ya Matiang’i,” Dkt Ruto akaongeza.

Naibu Rais alisema juhudi za Dkt Matiang’i za kumsawiri kama tajiri wa kupindukia zimesaidia kufafanulia Wakenya maana halisi ya “hustler.”

Dkt Ruto alieleza kuwa neno hilo lina maana kuwa mtu anaweza kuinuka kutoka maisha ya umasikini hadi kuwa mtu wa hadhi ya Naibu Rais “na hivyo kuzungumziwa katika vyombo vya habari.”

“Sasa Wakenya wameelewa kuwa mtu ambaye alivalia kiatu kwa mara ya kwanza akiingia kidato cha kwanza anaweza kuwa Naibu Rais na mali yake kujadiliwa katika vyombo vya habari. Hiyo ni kielelezo chema kwa mahasla wengine,” akasema.

Dkt Ruto alifafanua kuwa sio lazima mtu awe masikini ndio aitwe hasla. Kulingana naye, hasla ni mtu yule ana uwezo wa kupata mali kutokana na bidii yake wala sio zile ambazo amerithi kutoka kwa “wazazi wake wenye majina makubwa.”

You can share this post!

Polisi sita wakana kuua ndugu wawili Embu agosti 1, 2021

Yaibuka Ruto aligawia Jumwa GSU wawili ilhali ana kesi