Habari Mseto

Ninavuta bangi ili kuimarisha maarifa, mwanamume aambia korti

September 3rd, 2018 1 min read

Na Stephen Munyiri

MWANAMUME mmoja alivunja watu mbavu katika mahakama moja ya Karatina, Kaunti ya Nyeri Jumatatu, baada ya kueleza korti kuwa huwa anavuta bangi ili kufikiria kwa makini.

Akikiri kosa la kuvuta dawa hiyo ya kulevya, Bw Francis Mwangi Maina alieleza Hakimu Mkuu Mwandamizi Florence Macharia kuwa bangi imekuwa ikimsaidia kuwaza kwa utaratibu na kuwa haikumdhuru.

Mshukiwa alituhumiwa kupatikana na bangu gramu 50 mnamo Septemba 2 mjini Karatina, ambayo haikuwa na mapendekezo ya daktrari ili kutumika kama dawa.

“Mheshimiwa ninakubali kuwa nilipatikana na bangi lakini sababu ya kuitumia ni kwa kuwa huwa inanifanya kufikiria kwa makini na kufanya kazi yangu kwa umakinifu,” Bw Maina akaeleza korti.

Mwanamume huyo ambaye hufanya kazi za vibarua sasa atakumbana na hukumu ya makossa hayo Septemba 17, baada ya korti kutoa muda afanyiwe uchunguzi kubaini tabia yake na ikiwa yuko tayari kurekebika.