Habari

Ninavuta bangi ili nipate nguvu za kuchapa kazi shambani, mshukiwa aambia mahakama

April 19th, 2018 1 min read

Na STEPHEN MUNYIRI

MWANAMUME aliyekamatwa akiwa na bangi, Jumatano aliishangaza mahakama moja mjini Karatina, alipomwambia hakimu kwamba huwa inamsaidia kufanya kazi kwa bidii anapoivuta.

Mshukiwa huyo, Erick Njogu alikubali makosa hayo, mbele ya Hakimu Mkuu Florence Macharia.

“Nakubali kwamba mashtaka hayo ni ya kweli. Nilipatikana na bangi. Huwa ninaitumia kwani huwa inanisaidia kufanya kazi kwa bidii katika shamba langu,” akamwambia hakimu huyo, aliyeonekana kushangazwa na kauli hiyo.

Baadaye hakimu alimuuliza: “Je, unakubali uliyoyasema?” Mshukiwa alikubali bila kupepesa. Kauli yake ilizua gumzo kwa muda, hasa miongoni mwa viongozi wa mashtaka.

Upande wa mashtaka uliiambia mahakama kwamba mnamo Aprili 12, polisi walipata habari kutoka kwa wananchi kwamba mshukiwa amekuwa akiuza bangi.

Walibaini hayo kuwa kweli, baada ya kuvamia makazi yake, kwani walipata misokoto ya bangi yenye thamani ya Sh170.

Mahakama iliagiza afanyiwe ukaguzi, huku hukumu yake ikitarajiwa kutolewa mnamo Aprili 30.