Siasa

Ningekuwa Rais Wakenya tungekuwa mbali sana – Raila

January 25th, 2024 4 min read

NA WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga katika ziara yake ya Pwani amesema kama angeshinda urais, Wakenya wangefurahia sana utawala wa serikali ya Azimio La Umoja-One Kenya.

Alianzia ziara yake katika Kaunti ya Lamu mnamo Jumatatu ambapo alidai kwamba alipokonywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Lamu kuwa kama Dubai

Akiwa Lamu, Bw Odinga alidai kwamba ‘kunyimwa’ ushindi na ‘kudhulimiwa’ kwake kwenye uchaguzi mkuu kulileta kizingiti kikuu kilicholemaza mpango wake wa kuigeuza Lamu kuwa Dubai ndogo, hasa kimaendeleo.

Akihutubia wafuasi wake kwenye eneo la mikutano la Mkunguni kisiwani Lamu, Bw Odinga, ambaye alikuwa ameandamana na viongozi wakuu wa Pwani na wakuu wa chama cha ODM, alisema kwa ushirikiano wake na Rais Mstaafu, hayati Mwai Kibaki walianzisha Mradi wa Bandari ya Lamu na Miundomisngi ya Uchukuzi wa Kusini mwa Sudan na Ethiopia (Lapsset), lengo kuu likiwa ni kupanua Lamu na eneo zima la Kaskazini mwa Kenya kimiundomisngi na maendeleo.

Bw Odinga alisisitiza kuwa endapo angechaguliwa Rais wa Kenya kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9,2022, lengo lake kuu lilikuwa ni kujenga reli ya kisasa (SGR) ambayo ingeunganisha Lamu na mataifa jirani,ikiwemo Ethiopia na Sudan.

Bw Raila vile vile alisema azma yake ilikuwa ni kuweka barabara za kisasa zitakazorahisisha uchukuzi, hasa wa samaki na rasilimali nyingine na kuboresha viwanda eneo hilo.

Mbali na kuboreshwa kwa miundomisngi, Bw Odinga alisema dhamira yake endapo angechaguliwa Rais 2022 pia ilikuwa ni kujenga viwanja vya kisasa vya ndege na viwanda ili kuona kwamba Lamu inapanuka, hasa kimaendeleo, biashara na kuinua maisha ya wakazi kwa jumla mfano wa wanaoishi Dubai.

“Hii Lamu, kupitia Mradi wa Bandari (Lapsset) nilikuwa nimepanga kuiendeleza na kuigeuza kabisa kuwa Dubai Ndogo. Kura zikapigwa, tukashinda lakini tukanyimwa ushindi wetu. Leo hii Mungu halali. Mnaona vile uongozi wako nao lakini unawanyonga. Wananchi wanateseka kwa gharama ya juu ya maisha lakini walioko utawalani hawawezi kusaidia. Lazima tusimame imara kuikomboa nchi hii kutoka kwa wanasiasa potofu,” akasema Bw Odinga.

Wakati wa hotuba yake, Bw Odinga alichukua fursa hiyo kuwarai wakazi wa Lamu, Pwani na nchini kwa ujumla kujitokeza kwa wingvi na kujisajii kuwa wanachama kindakindaki wa ODM ili kuwawezesha kushindana ipasavyo ifikapo Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Tumefika Lamu kuwahimiza wananchi wote kuamka na kujisajili kwa wingi kuingia ODM. Tuko tayari. Tusimame imara ili kutetea ushindi wetu ifikapo 2027,” akasema Bw Odinga.

Kauli yake iliungwa mkono na Katibu wa Chama cha ODM, Edwin Sifuna aliyesema ili chama cha ODM na mrengo wa Azimio La Umoja kuwa na nguvu zaidi, lazima wananchi wajitokeze na wasimame imara kujisajili kuwa wanachama kamili wa ODM.

Wengine walioandamana na Bw Odinga kwenye ziara ya Lamu ni Gavana wa zamani wa Kakamega, Wyclife Oparanya, Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko, Mbunge wa Jomvu, Bw Badi Twalib, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake kaunti ya Mombasa, Bi Zamzam Mohammed, madiwani wa Mombasa na Lamu na viongozi wengine.

Tana River

Jumanne ilikuwa siku ya pili ya ziara yake Pwani ambapo kiongozi huyo wa ODM alisema kuwa mbunge Junet Mohamed (Suna Mashariki) hataondoka katika chama hicho.

Bw Odinga alikuwa akirejelea ripoti kwamba kuna mipango ya kumwadhibu kiongozi huyo, kutokana na mtindo wake wa kukwepa vikao muhimu vya chama hicho.

Ripoti hizo mnamo wikendi zilieleza kuwa tayari, chama hicho kimemwandikia barua ya kumchukulia adhabu mbunge huyo.

Pia, zilieleza kuwa chama kimetishia kumwondoa kama Kiraja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa.

Lakini Jumanne, Bw Odinga alitaja ripoti hizo kama “ propaganda zinazoenezwa na vyombo vya hanbari”.

Akihutubu katika Kaunti ya Tana River, Bw Odinga aliwarai wafuasi wake kote nchini kuzipuuza.

“Junet hajaenda mahali. Haendi mahali. Huo ni uvumi unaoenezwa na vyombo vya habari. Nyumba iliyo na bwana na bibi haiwezi kukosa tofauti za kimaoni. Hayo ni mambo ya kawaida. Junet hajaenda mahali na hakuna mtu amemgusa. Ndiye Mkurugenzi wa Kampeni katika ODM na kiongozi katika muungano wa Azimio. Yale yote yanayoandikwa na magazeti ni propaganda,” akasema Bw Odinga.

Bw Odinga alisema ripoti ambazo zimekuwa zikiandikwa dhidi ya kiongozi huo ni “ubunifu wa vyombo vya habari”.

Alisema kuwa ripoti hizo zinafanana na madai kwamba mrengo wa Azimio unakumbwa na migawanyiko.

Kwa muda mrefu, Junet amekuwa miongoni mwa washirika wa karibu zaidi wa Bw Odinga.

Kutokana na ukaribu huo, alikuwa baadhi ya wanasiasa walioongoza kampeni za urais za Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Hata hivyo, baada ya Bw Odinga kutoshinda urais kwenye uchaguzi huo, kiongozi huyo amekuwa kimya, ikilinganishwa na hapo awali.

Baadhi ya viongozi katika mrengo huo wamekuwa wakimlaumu mbunge huyo kwa kuchangia pakubwa Bw Odinga kutoibuka mshindi kwenye uchaguzi huo.

Raila asuta Rais Ruto na Koome

Akihutubia wajumbe wa ODM mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi mnamo Jumatano, Bw Odinga alisema ofisi ya Rais, inaendelea kuziteka nyara asasi muhimu za serikali, ambazo zinafaa kufanya kazi bila mwingiliano wa aina yoyote, kwa mujibu wa sheria.

Bw Odinga alidai kwamba Rais anavuruga mahakama, Bunge la Kitaifa na lile la Seneti kwa kushinikiza asasi hizo kupitisha miswada bila kuipiga msasa vilivyo.

Kuhusu mazungumzo yaliyofanyika Jumatatu baina ya ofisi ya Rais na Mahakama katika Ikulu, ambapo pia Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alihudhuria, Bw Odinga alisema yaliendeshwa kiharamu.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga (wa tatu kulia) akiwa na viongozi wengine wa chama hicho wakati wa hamasisho la usajili wa wanachama katika eneo la Marafa, Kaunti ya Kilifi mnamo Januari 24, 2024. PICHA | KEVIN ODIT

Alifafanua kwamba endapo kulikuwa na kashfa yoyote katika idara ya mahakama, kulikuwa na njia nyingine za kukabili hali hiyo.

“Zipo njia muafaka za kuleta mageuzi katika Idara ya Mahakama na njia hizo ni kutumia taasisi huru au tume maalum na wala sio Rais, mahakama na bunge,” akasema Bw Odinga.

Kiongozi huyo ambaye pia ni kinara wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya, amedai kuwa mabunge yote mawili–la kitaifa na seneti–yameshikwa mateka na afisi ya Rais, na huendesha shughuli zao kinyume na sheria.

“Wabunge wanapitisha kila kitu ambacho kinatoka kwa Ikulu. Hakuna chochote ambacho kinabadilishwa. Miswada inapenyezwa tu bungeni na spika anaamua kwamba ni sharti ipitishwe kwa muda wa saa mbili. Hakuna kinachojadiliwa… huwezi ukajadili mswada kwa saa mbili,” akasema.

Bw Odinga hakuwasaza maspika wa mabunge hayo mawili, akisema kuwa wamekuwa wakikiuka sheria kwa kuhusishwa wakati wa Rais kutia saini miswada kuwa sheria.

“Spika hana wajibu wowote baada ya mswada kutoka bungeni. Siku hizi ninaona maspika wa Seneti na Bunge la Kitaifa wakienda kwa Ikulu na kusimama wakishuhudia Rais akitia saini miswada. Aibu kwao!” akasema.

Leo Alhamisi Bw Odinga atazuru Kwale.

Mnamo Ijumaa atakuwa Taita Taveta kisha Jumamosi akamilishe ziara yake katika Kaunti ya Mombasa.

Ripoti za Kalume Kazungu, Alex Kalama na Wanderi Kamau