Nini hasa ndicho kiini cha mtu kujitia kitanzi?

Nini hasa ndicho kiini cha mtu kujitia kitanzi?

Na MWANGI MUIRURI

KUAMUA kujiua kumehusishwa sana na shida ya kiakili. Kuna wadadisi ambao hushikilia kuwa shida hiyo ambayo huishia kuwa hitilafu ya kimawazo huanza na msongamano wa kimawazo ndani ya bongo kiasi cha kuishia kusombwa na kulemewa na hayo mawazo.

Lakini ukizingatia jinsi wengi hujiua, utapata kwamba hata ikiwa kulikuweko na hizo hitilafu za kimawazo, mpangilio wa matukio ya kuishia kujigeuza maiti huwa na utimamu wa kuakili.

Utapata mtu hata alijificha wenzake, akajipa umilisi wa kamba au kemikali kujiua na bila kufanya masihara na shughuli hiyo, wanazimba mianya yote ya kukosa kufanikisha kujiua.

Ndipo kunaashiriwa kuwa huenda kuna uwezekano kuwa kujiua huwa ni maamuzi ya mtu binafsi akiwa na ufahamu na hiari ya mauti.

Ndipo uchambuzi uzingatie kisa na matukio ya hivi majuzi katika Kaunti ya Murang’a bapo kijana wa miaka 39 alijitoa uhai baada ya kupandwa na hasira ya kunyimwa pesa za kununua pombe na bibi yake.

James Kamau kutoka kijiji cha Mbogo-ini kilichoko katika wadi ya Kahumbu anasemekana kuwa aliafikia uamuzi huo na kuwaacha wengi katika hali ya mshangao kuwa pesa za ulevi zinaweza zikamsukuma mtu kujidhulu kwa kiwango cha kujiua.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Murang’a, Josephat Kinyua mwanamume huyo alikuwa ameshida katika mtaa wa Mbogo-ini akitoa miche za parachichi ambazo serikali ya kaunti hiyo inapea wakulima.

‘Kuna mradi wa gavana Mwangi wa Iria ambao unalenga kutoa miche milioni moja kwa wakulima 250, 000 wa kaunti hiyo. Bw Kamau ambaye tunaongea kuhusu kujiua kwake ndiye alikuwa akishirikisha utoaji wa miche hiyo katika mtaa huo,” akaambia Taifa Leo.

Aliongeza kuwa Bw kamau hata yeye alijipa miche kadhaa na ambayo alichukua kibarua mmoja na wakaandamana naye hadi shambani lake na wakaipanda.

“Ndipo Bw kamau aliamua kuburudika katika baa moja ambayo iko karibu na nyumbani kwake. Aliandamana na yule kibarua wake…Walinunua lita mbili za pombe aina ya Senator Keg na Kamau ndiye aligharamia,” asema.

Kamanda huyo aliongeza kuwa duru za mashahidi ziliarifu kuwa “ni kama Bw Kamau hakutosheka na pombe hiyo na akawa amemaliza pesa alizokuwa amebeba.”

Ndipo, yaripotiwa, alitoka na akarejea nyumbani mwendo wa saa nne usiku na akamuomba bibi yake pesa.

“Bw kamau amekuwa mfanya biashara ambaye katika siku za hivi karibuni haikuwa ikiwmendea vyema. Naye bibi yake huwa na duka la kuuza bidhaa…Inasemwa kuwa bibi alikataa kutoa pesa za kufadhili ulevi,” akasema Bw Kinyua.

Ndipo kwa hasira Bw Kamau alizua fujo akitaka apewe pesa kwa lazima.

“Tumepata taarifa kuwa baada ya mamake Kamau kusikia vurugu hilo, alikimbia na akadadisi hali akaona fujo hizo zilikuwa na ukali mwingi…Mamake Kamau alimchukua bibi huyo na akampa malazi..Kwa hasira, kamau alisikika akionya mamake kuwa alikuwa na mapendeleo kwa bibi huyo na akaapa kuwaadhibu wote wawili kwa maombolezi,” asema kamanda huyo.

Inaarifiwa kuwa Bw Kamau alirejea kwa nyumba yao ambapo watoto wao watatu walikuwa usingizini, akafunga mlango na asubuhi yake watoto walipoamka, wakamwona baba yao akining’inia kutoka kwa paa la nyumba sebuleni.

Walifungua mlano na kutoa habari hizo na ndipo ilibainika kuwa Bw Kamau tayari alikuwa marehemu na ambaye alipelekwa hadi Mochari ya Murang’a kuhifadhiwa.

Hayo yakawa masaibu ya kusombwa na mawazo, kujaribu kuyatuliza kwa ulevi na kufeli, kijisababu cha kunyimwa pesa ba mkewe kikatumika kama basi la kujisafirisha hadi kuzimu—janga la kijamii.

Na ndipo ukizingatia matukio hayo, unaulizwa: Je, Kamau alikuwa na sababu halali ya kujiua?

You can share this post!

Mzee Kenyatta alituchezea shere kuhusu mashamba, wasema Mau...

Kaunti yafadhili familia 16,870 kwa NHIF

adminleo