Michezo

NIPE NIKUPE: Manchester United mizanini ikiwazuru Wolves kwa pambano la EPL

April 2nd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

MSHAMBULIAJI Anthony Martial hatakuwa sehemu ya kikosi cha Manchester United kitakachomenyana leo na Wolves kwenye mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Molineux.

Martial ambaye amekuwa nguzo kubwa katika kampeni za waajiri wake msimu huu, anauguza jeraha la mguu linalotarajiwa kumweka mkekani kwa kipindi cha majuma mawili yajayo.

Kwa mujibu wa kocha Ole Gunnar Solskjaer, mvamizi huyo mzawa wa Ufaransa aliondolewa uwanjani kunako dakika ya 77 katika mchuano wa EPL uliowakutanisha na Watford mwishoni mwa wiki jana kwa sababu ya jeraha.

Manchester United walisajili ushindi wa 2-1 katika mechi hiyo iliyopigiwa ugani Old Trafford na kupaa jedwalini hadi nafasi ya nne kwa alama 61.

Ingawa ufanisi huo wa Man-United unatarajiwa kuwatambisha zaidi katika mchuano wa leo, Solskjaer amewaonya masogora wake dhidi ya utepetevu.

Ugumu wa mtihani wa leo Jumanne wa Man-United ni ubabe wa Wolves ambao wamefaulu kuwaangusha miamba wa soka ya Uingereza hadi kufikia sasa muhula huu.

Baada ya kuwalazimishia Man-City sare ya 1-1 mnamo Agosti 2018, Wolves walisajili matokeo sawa na hayo katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa EPL dhidi ya Man-United uwanjani Old Trafford.

Isitoshe, waliambulia sare ya 1-1 na Arsenal mnamo Novemba 11, 2018 kabla ya kuwaduwaza Chelsea kwa kichapo cha 2-1 uwanjani Molineux mwanzoni mwa Disemba.

Baada ya kuwalazimishia Chelsea sare ya 1-1 katika mkondo wa pili mnamo Machi 10, kikosi hicho cha mkufunzi Nuno Espirito Santo kiliwabandua Man-United kwenye robo-fainali za Kombe la FA wiki moja baadaye.

Mchuano wa leo utakuwa wa sita kwa Martial kukosa kuwachezea Man-United msimu huu tangu alipoanza kusumbuliwa na jeraha la paja mwezi mmoja uliopita.

Mwishoni mwa wiki jana, nyota huyo wa zamani wa AS Monaco nchini Ufaransa, alifunga bao la pili la Man-United dakika tano kabla ya nafasi yake kutwaliwa na beki mzaliwa wa Argentina, Marcos Rojo.

Licha ya kuhusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Real Madrid, Paris Saint-Germain (PSG) au Bayern Munich, Martial alitia saini mkataba mpya wa miaka mitano kambini mwa Man-United mwezi Machi.

Kwa pamoja na Paul Pogba na Marcus Rashford, Martial ni miongoni mwa wachezaji ambao kwa sasa wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya kocha Solskjaer aliyepokezwa mkataba wa kudumu na waajiri wake wiki moja iliyopita.

Kulingana na Solskjaer, huenda kikosi chake kikatumia mfumo wa 4-4-2 dhidi ya Wolves ambao wana kiu ya kujinyanyua baada ya kuzimwa 2-0 na Burnley wikendi jana. Pogba, Nemanja Matic na Ander Herrera wanatazamiwa kushirikiana na Jesse Lingard katika safu ya kati huku Rashford na Romelu Lukaku wakitegemewa katika idara ya uvamizi.

Ratiba ya EPL (Leo Jumanne):

Wolves na Man-United
Watford na Fulham

(Jumatano):

Chelsea na Brighton
Tottenham na Palace
Manchester City na Cardiff