Michezo

Nitaangika glovu Porto nikigonga miaka 40 – Casillas

March 19th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

‘NYANI’ veterani wa mibabe wa soka nchini Ureno, FC Porto Iker Casillas amesema analenga kusakata kabumbu hadi ahitimu umri wa miaka 40.

Nyota huyo vile vile amefichua kwamba atastaafu taaluma yake ya soka akiwajibikia timu hiyo aliojiunga nayo kutoka Real Madrid.

Casillas ambaye ana umri wa miaka 37 ameimarika sana na kugandia nafasi ya mlinda wa Porto msimu wa 2018/19, hilo likidhihirika baada ya kuanza mechi 34 kwenye ligi, Klabu Bingwa Bara Uropa(UEFA) na mashindano mengine nchini Ureno.

Mnyakaji huyo majuzi alimwaga wino kwenye mkataba nene unaoongeza muda wake wa kuchezea FC Porto kwa mwaka moja akiwa kwenye msimu wake wa tano tangu ajiunge nayo.

Kuongezwa kwa muda huo kutamweka kambini mwa timu hiyo hadi mwaka wa 2022.

“Tangu nitue hapa Ureno na kujiunga na kambini mwa FC Porto, Rais wa klabu hii Pinto da Costa amenishughulkia vizuri na tena kwa heshima ya juu. Wiki hii nitatia kandarasi itakayoniweka FC Porto hadi nihitimu miaka 40. Kwa sasa nina miaka 37 na kuna dalili za kutosha kwamba nitakamilisha taaluma yangu ya soka hapa FC Porto,” Casillas akaeleza kwenye mtandao wa klabu.

Jagina huyo amejizolea sifa kedekede katika kipindi ambacho amekuwa kwenye ulingo wa soka baada ya kuongoza Uhispania kushinda Kombe la Dunia mwaka wa 2010 na pia kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Barani Uropa(UEFA) mara tatu akichezea Real Madrid ya Uhispania.