Bambika

Nitaanza kutoka na vibenten kwa jinsi mnavyonisema, atishia DJ Pierra Makena

January 9th, 2024 1 min read

NA RAJAB ZAWADI

DJ Pierra Makena, mmoja wa washereheshaji wakongwe hapa nchini anakiri wazi wazi kwamba mashabiki na wafuasi wake wameanza kumfanya kuwaza kutaka kutoka na vijana wadogo.

Ishu ipo hivi, Dj Pierra mwenye miaka 42 kwa sasa, amekuwa akionyesha ukaribu wa sana na mtaalamu wa upodozi dogo Creative Phil.

Mara kwa mara wamekuwa wakiachia picha za pozi za kichokozi ambazo wengine wameishi kujijazia kuwa watakuwa ni wapenzi.

Na licha ya Pierra kusisitiza kuwa yule bwana mdogo ni mshikaji wake wa sana tu na kwamba hamna la ziada kati yao zaidi ya mapenzi ya ubeste, wengi wamekuwa wakihisi mrembo huyo atakuwa anawapaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Sasa juzi akipiga stori pale Insta na mashabiki zake zaidi ya laki nane, Pierra amekiri kuwa msukumo wa kutaka kutoka kimapenzi na vi-ben ten umezidi sana kutoka kwao na sasa ni kama vile ameanza kuwaza kulifanyia kazi.

“Jamani eeh naombeni mtulie, munatunga sana stori zisizo za kweli. Hamjui mnaweza kuniweka kwenye utata na mtu niliye naye, mtanivunjia nyumba. Au ndio kusudi leo. Lakini kikweli niwe muwazi kwa msukumo wenu huu, nahisi pengine ikitokea naweza kutoka kimapenzi na hawa mastaa wachanga.”

Hata hivyo, DJ Pierra kwa sasa anasisitiza yupo kwenye mahusiano mazuri tu na mpoa wake lakini ikija kutokea penzi limeisha basi wazo la kutoka na watoto wadogo wanaotosha kuwa wanawe, hatalizuia.