Michezo

Nitachapa kazi na wanaotii amri zangu – Arteta

July 5th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Mikel Arteta amesema atafanya kazi na wanasoka watakaoafikiana naye kimawazo pekee kadri anavyopania kurejesha hadi ya kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza.

Kauli ya Arteta ilichochewa na tukio la hivi majuzi ambapo kiungo mzawa wa Ufaransa, Matteo Guendouzi, 21, aliwasilisha ombi la kutaka kuagana na Arsenal mwishoni mwa msimu huu baada ya kutupwa nje ya kikosi kilichosajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Southampton uwanjani St Mary’s.

Arteta alisema hatua ya kuachwa nje kwa Guendouzi ilichangiwa na haja ya ‘kumdhibiti’ baada ya kuzua rabsha alipovurugana na fowadi Neal Maupay wa Brighton katika mechi ya awali iliyomshuhudia kipa Bernd Leno akipata jeraha baya la mguu.

“Wachezaji wote waliopo hapa ni wale ambao natarajia kwamba nitawategemea kila wakati kwa kuwa wanaafikiana nami kwa kila jambo. Iwapo haiwezekani kusafiri na baadhi yao katika boti yangu, basi itabidi tuchukue hatua,” akatanguliza Arteta.

“Ni wajibu wangu kumsaidia kila mchezaji kujiboresha na hatimaye kuimarisha kikosi kizima,” akaendelea kocha huyo mzawa wa Uhispania.

Kwa kuwa Guendouzi hakuadhibiwa na Shirikisho la Soka la Uingereza (FA), Guendouzi huenda akawajibishwa katika robo-fainali ya Kombe la FA dhidi ya Sheffield United mnamo Juni 28 uwanjani Bramall Lane.

Kutochezeshwa kwa Guendouzi dhidi ya Southampton kulimpa nafasi kiungo Granit Xhaka aliyerejea ugani baada ya kupona jeraha alilolipata dhidi ya Manchester City mnamo Juni 17, 2020.

Xhaka, 27, alipokonywa utepe wa unahodha wa Arsenal na kocha Unai Emery mnamo Oktoba 2019 baada ya kuvurugana na mashabiki katika mechi iliyowashuhudia wakiambulia sare ya 2-2 dhidi ya Crystal Palace uwanjani Emirates.

Hata hivyo, Arteta hajabainisha iwapo kiungo huyo mzawa wa Uswisi atarejeshewa ukapteni ambao kwa sasa unashikiliwa na mvamizi matata mzawa wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang.

“Ni kiongozi wa kujituma sana na kiwango chake cha kujitolea kila anapokuwa uwanjani ni zaidi ya asilimia 1,000,”akasema Arteta.