Makala

Nitaendelea kutetea masilahi ya mtoto mvulana hata bila bajeti – Pasta Dorcas Gachagua 


MKEWE Naibu Rais, Rigathi Gachagua, Pasta Dorcas Rigathi ameapa kuendelea na mipango na miradi yake ya kuendeleza masilahi ya mtoto mvulana licha ya serikali kuondoa bajeti ya afisi yake.

Aidha, ameahidi kuendelea na mipango yake ya kusaidia waraibu wa pombe haramu, sio tu eneo la Mlima Kenya bali kote nchini.

Akiongea Jumapili, Julai 7, 2024 katika Kanisa la PEFA, eneo la Kiamariga, Kaunti ya Nyeri, Pasta Dorcas alifichua kuwa alianza mipango hiyo hata kabla ya mumewe kuchaguliwa kuwa Naibu Rais.

“Ni sawa kwamba Wakenya hawataki Mkewe Naibu Rais kutengewa bajeti kufadhili mipango yake. Lakini nawahakikishia kuwa nitaendelea kupigania masilahi ya mtoto mvulana hata bila mgao wa bajeti,” akasema.

Alieleza kuwa ataendelea kufadhili mipango hiyo, ikiwemo ile ya kusaidia waathiriwa wa uraibu wa pombe, kwa kutumia fedha zake mwenyewe na “misaada kutoka kwa wahisani.”

“Mpango huu ni zao la ndoto na matamanio niliyo nayo kusaidia mtoto mvulana. Sitausitisha kwa sababu niliuanza hata kabla ya serikali hii kuingia afisini. Naamini kuwa ninyi na mimi tutaiwezesha kufaulu,” Pasta Dorcas akaelezea.

Ijumaa wiki jana, Rais William Ruto alifutilia mbali mgao wa bajeti kwa afisi ya Mkewe, Rachel Ruto, Pasta Dorcas (Mke wa Naibu Rais) na mke wa Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, Tessie Mudavadi.

Dkt Ruto alisema hiyo ni sehemu ya hatua za kupunguza matumizi ya serikali baada ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 uliopelekea serikali kupoteza mapato ya kima cha Sh346 bilioni.

Katika makadirio ya bajeti yaliyosomwa na Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u, Bungeni mnamo Juni 13, 2024, Afisi ya Bi Ruto na Afisi ya Bi Gachagua zilitengewa jumla ya Sh1.2 bilioni kufadhili shughuli yazo kuanzia Julai 1, 2024 hadi Juni 30, 2025.

Kwa mujibu wa mgao huo, Afisi ya Bi Ruto ingepata Sh696.6 milioni huku ile ya Bi Gachagua ikipata Sh557.5 milioni.