Habari MsetoSiasa

Nitafuata masharti yote – Obado

October 26th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

GAVANA wa Migori Okoth Obado ameahidi kufuata masharti makali iliyompa korti wakati ilipomwachilia huru kwa dhamana, na kuahidi kuanza kuchapa kazi huko Migori.

Kupitia ujumbe kwenye ukurasa wake wa Facebook Ijumaa asubuhi, saa chache baada ya kupata uhuru, Gavana Obado alishukuru mahakama kwa kumpa uhuru akisema sasa hiyo ni fusra kwake kuanza kufanyia wakazi wa Migori kazi.

“Wacha nichukue fursa hii kuwashukuru watu wa Migori, Wawakilishi wadi wa Migori, wafanyakazi wa serikali ya kaunti, wafuasi wangu, mawakili, marafiki na familia kwa kusimama name wakati huu mgumu.

Pia naishukuru korti kwa kusikia maombi yetu na kunipa dhamana. Hii sasa imenipa fursa ya kuwafanyia kazi watu wa Migori kama gavana wao,” Bw Obado akachapisha.

“Ninaahidi kuheshimu korti na kufuata masharti iliyoweka. Ninawarai viongozi wote, bila kujali kabila ama mirengo ya kisiasa kudumisha amani na umoja ili kama familia tuendeleze ajenda ya maendeleo ya kaunti yetu. Asanteni sana na Mungu awabariki nyote,” gavana huyo akasema.

Huu ulikuwa ujumbe wake wa kwanza kwa umma tangu alipokamatwa zaidi ya mwezi mmoja uliopita, na kuzuiliwa rumande katika jela ya Industrial Area aliposhtakiwa na makosa ya mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Sharon Otieno.

Alipomwachilia kwa dhamana ya Sh5milioni na wadhamini wawili wa kiasi sawa, Jaji Jessie Lesiit alimtaka Bw Obado kuripoti kwa msajili wa Mahakama za Milimani mara moja kila mwezi, kupeana hati zake za usafiri kwa mahakama, kutozungumzia sulala la kesi hiyo katika hafla za umma ama kukanyaga popote ndani ya kilomita 20 kati ya mpaka wa kaunti za Migori na Homa Bay.