Nitagura Jubilee kwa hiari ila si kwa kushurutishwa – Ruto

Nitagura Jubilee kwa hiari ila si kwa kushurutishwa – Ruto

Na SAMMY WAWERU

LICHA ya wapinzani wa Naibu wa Rais William Ruto kumtaka atangaze kujiuzulu rasmi katika chama tawala cha Jubilee (JP), amesema atakigura kwa hiari ila si kwa njia ya kushurutishwa.

Wakosoaji wake wamekuwa wakimtaka aondoke chamani, badala ya kuendelea kuitoa makosa serikali inayoongozwa na chama kilichomuingiza madarakani.

Dkt Ruto alisema Alhamisi yeye si mgeni katika JP na licha ya kuonekana kutengwa ni uamuzi wake kukaa au kuondoka.

“Sisi si wageni popote. Huwa tunajiunga na vyama kwa hiari na kuviondoka kwa hiari.

Hakuna anayepaswa kusumbuka au kuuliza kwa nini unaendelea kusalia ulipo. Watu hufanya maamuzi wakati ufaao na endapo yanafaa,” Ruto akafafanua.

Alisema hayo baada ya kukutana na zaidi ya wabunge 100 wanaohusishwa na chama kipya cha UDA.

Aidha, UDA pia inahusishwa na Dkt Ruto.

Wabunge waliozungumza baada ya mkutano huo wa faragha, walisema Jubilee ni chama ambacho tayari kimeanguka kufuatia kile walitaja kama kuasi sera zake.

Nyufa zinaendelea kushuhudiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Ruto, hasa baada ya Rais na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga kutangaza kuzika tofauti zao kisiasa kupitia mapatano ya Handisheki, Machi 2018.

You can share this post!

Kenya na TZ kurahisisha upimaji corona

Wanafunzi wanaougua corona hawaonyeshi dalili – Kagwe