Nitajenga kwangu kasri la kula na kunywa – Rigathi

Nitajenga kwangu kasri la kula na kunywa – Rigathi

NA STEPHEN MUNYIRI

MWANIAJI mwenza wa Urais wa Muungano wa Kenya Kwanza Rigathi Gachagua amezua kioja tena kwa kuahidi kujenga jumba la kifahari nyumbani kwake ambako atashiriki sherehe ya kunywa na kula nyama akitangamana na wafuasi wake.

Bw Gachagua ambaye pamoja na Naibu Rais Dkt William Ruto wanawania uongozi wa nchi kupitia tikiti ya UDA, pia alisema mkewe atakuwa akiandaa mikutano na makundi ya wanawake na kushiriki burudani katika kasri hilo alilofananisha na ikulu

“Nitajenga nyumba nzuri katika wadi hii ya Konyu ambapo tutakuwa tukiburudika kwa kunywa na kula nyama pamoja na wanaume wa hapa.

Mke wangu pia atakuwa na sehemu ambapo atakuwa akikutana na makundi ya wanawake hapa,” akasema Bw Gachagua akizungumza katika wadi ya Konyu, eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri.

Katika siku za hivi karibuni, Bw Gachagua amekuwa akimulikwa kwa kutoa matamshi ya kutatanisha yanayoonekana kuwakera hata wafuasi wa UDA, baadhi hata wakijuta kwa nini Dkt Ruto alimteua mgombeaji mwenza wake badala ya Seneta wa Tharaka-Nithi, Profesa Kithure Kindiki.

Mwezi uliopita, Bw Gachagua alikaangwa mitandaoni kwa kumtaka Dkt Ruto arejeshe hafla za kifahari za burudani katika ikulu jinsi ilivyokuwa enzi za utawala wa marehemu Rais Daniel Moi. Alisema Wakenya watakuwa wakitumia hafla hizo kunywa na kula pamoja na viongozi wao. Wakati wa mazishi ya ndugu yake wa kambo katika kijiji cha Hiriga yaliyohudhuriwa na Dkt Ruto, Bw Gachagua alimtaka bosi wake afungue ikulu ndogo na maeneo ya burudani kwa umma ili awachinjie mbuzi na fahali ndipo wafurahie pamoja.

Kabla ya hilo kusahaulika, Bw Gachagua alizua utata tena kwa kudai kuwa sare ya sasa ya polisi itaondolewa kwa sababu inafanana na nguo zinazovaliwa na wanawake wa kanisa la PCEA.

Alidai rangi hiyo ya samawati mwanzoni ilikuwa ya kitengo cha wanawake wa PCEA. Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho na baadhi ya viongozi walimkashifu Dkt Kibicho kwa kudharau idara ya polisi.

Pia, alijipata matatani siku chache baada ya kupokezwa hadhi ya mgombeaji mwenza wa Dkt Ruto kwa kudai atafunga kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kisha kufungua kampuni nyingine ndogo ambazo zitatoa nafasi za ajira kwa wengi na kulipa ushuru mwingi.

Licha ya matamshi hayo, Dkt Ruto amelazimika mara kadhaa kujitokeza na kujitetea akiwakashifu wapinzani wao kwa kugeuza matamshi ya Bw Gachagua na kuyatumia kusaka uungwaji mkono kisiasa. Isitoshe alidai kuwa ataongeza mchango anaotoa kanisani kutoka Sh100,000 hadi Sh1 milioni iwapo atachaguliwa kwa sababu mshahara wake utakuwa mkubwa akiwa Naibu Rais.

Vilevile alisema kuwa akaunti zake zenye Sh2.5 bilioni ambazo zilifungwa kutokana na ufisadi zitafunguliwa akiingia mamlakani pamoja na Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Farm shield: Kifaa kinachorejelewa kama ubongo wa shamba

Shirika la feri lakubali lawama kuhusu ajali

T L