Michezo

Nitajituma kufa kupona hadi Harambee Stars waingie Kombe la Dunia Qatar 2022 – Wanyama

September 27th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAADA ya kuongoza Kenya kushiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri kwa mara ya kwanza tangu 2004, kiungo na nahodha wa Harambee Stars Victor Wanyama sasa ana malengo mapya ndani ya jezi za timu ya taifa.

Nyota huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur amesema kwamba hana nia ya kuangika daluga zake katika soka ya kimataifa hivi karibuni na kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuongoza Kenya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Ili kuweka hai ndoto hiyo, Harambee Stars ya Kenya italazimika kuwaangusha Mali, Uganda na Rwanda na kuibuka kileleni mwa Kundi E katika safari yao ya kujikatia tiketi ya kutua Qatar.

“Tumo katika kundi gumu na tunaheshimu kila kikosi. Hata hivyo, badala ya kuhofishwa na ubora wa viwango vya wapinzani, inatulazimu pia kujifua vilivyo na kuwabwaga kwa sababu hakuna lisilowezekana katika soka,” akatanguliza Wanyama.

“Mshindi wa mchezo wa soka huamuliwa uwanjani, si kwa kutegemea ukubwa wa majina ya wachezaji. Tuna kibarua cha kujitahidi kadri ya uwezo na kusajili matokeo ya kuridhisha katika hatua ya makundi.”

“Nadhani Mali ndio wanapigiwa upatu kwa sasa. Lakini Kenya, Uganda na Rwanda pia ni vikosi vizuri na yeyote kati yao ana uwezo wa kuduwaza Mali,” akasema.

“Ndoto ya kila mwanasoka ni kuwakilisha taifa lake kwenye fainali za Kombe la Dunia – shindano kubwa zaidi la hadhi katika ulingo wa kabumbu. Ni matumaini yangu kwamba mambo yatatuendea vizuri ili tufike Qatar 2022,” akaongeza Wanyama katika mahojiano yake na mtandao wa Fifa.com.

“Nimesafiri na kutua kwingi katika safari yangu ya kupiga soka ya kitaaluma. Nilianzia Kenya kisha Ubelgiji halafu Scotland nilikochezea Celtic. Baada ya hapo nilihamia Southampton halafu Tottenham kisha Montreal Impact nchini Canada,” akaongeza.

Kwa mujbu wa Wanyama, kilele cha usogora wake kilijiri wakati akivalia jezi za Spurs na hakuna tukio litakalosalia katika kumbukumbu zake milele kuliko kuongoza Spurs kushiriki fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Liverpool mnamo 2018-19 uwanjani Wanda Metropolitano, Madrid, Uhispania.

“Kusakata soka katika EPL kulinipa fursa ya kujifunza mengi kitaaluma chini ya aliyekuwa kocha wa Spurs, mkufunzi Mauricio Pochettino. Huko ndiko nilikofurahia zaidi usogora wangu. Ni tija na fahari tele kuwa sehemu ya wachezaji waliowahi kunogesha ligi bora zaidi duniani,” akaeleza Wanyama.

Baada ya kucheza soka barani Ulaya kwa zaidi ya miaka 10, Wanyama alihamia Montreal mwanzoni mwa 2020. Sogora huyo aliwajibishwa kwa mara ya kwanza katika kikosi ch Stars na kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee akiwa na umri wa miaka 15 pekee.

“Nakumbuka vizuri fursa hiyo niliyopewa na Mulee. Nilichezeshwa kwa dakika chache za mwisho wa mechi. Ingawa sikuridhisha sana, nilifurahi sana na kujifunza mengi,” akafafanua.

Baada ya kupokezwa malezi ya soka kambini mwa JMJ Youth Academy mnamo 2006, Wanyama alivalia jezi za Nairobi City Stars (2006) kabla ya kujiunga na AFC Leopards (2006-07). Aliyoyomea baadaye nchini Ubelgiji kuvalia jezi za Helsingborg (2007-08) na Beerschot (2008-11) kabla ya kutua Scotland kuchezea Celtic (2011-13).

Wanyama alielekea baadaye Uingereza kuchezea Southampton (2013-16) kabla ya kusajiliwa na Tottenham aliowawajibikia kuanzia 2016 hadi mwanzoni mwa 2020 alipoingia Montreal ya Canada inayonolewa na mwanasoka matata wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry.