Habari Mseto

Nitakosa mwanamume wa kunitongoza picha ikichapishwa, msichana aambia hakimu

August 8th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KIDOSHO aliyegeuka bondia  na kumzamba masumbwi  msichana katika kituo cha Reli Jumanne aliomba mahakama iamuru wanahabari wasipeperushe picha yake kwenye mitandao na kwenye magazeti kwa vile “mimi ni mseja. Sijaolewa na nitakosa mume.”

“Mheshimiwa naomba tu uamuru wanahabari hawa wasipeperushe picha yangu katika mitandao ya kijamii na kwenye magazeti. Nitakosa mtu wa kunioa. Mimi ni msichana tu,” Bi Yvonne Atieno Omondi alimsihi hakimu mkuu mahakama ya Milimani Francis Andayi.

Kidosho huyo alijifunika uso kwa bahasha lakini Bw Andayi akamwagiza aondoe bahasha kwenye uso ndipo auone uso wake.

“Nataka kuona uso wako. Nataka kujua ni mtu wa aina gani alifikishwa mbele yangu. Ukijificha uso nitakujua aje?” Bw Andayi alimweleza mshtakiwa.

Bw Andayi alimwuliza tena , “Ni kitu gani unaogopa?”

“Naogopa picha yangu kuchapishwa katika magazeti na kwenye mitandao. Sifa zangu zitaharibika. Mimi ni mseja. Sijaolewa na sifa zangu zitahabarika kabisa. Nitakosa wa kunitongoza,” alijibu Atieno.

“Ikiwa unaogopa picha na jina lako kuharibika basi uongee na Bi Edah Kwamboka Omwenga msuluhishe haya maneno mbali na wanahabari. Hautajulikana,” Bw Andayi alimshauri.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh20,000. Alikana alimchapa na kumwumiza Bi Omwenga katika  mzunguko wa barabara ya Stesheni ya Magari Moshi, Nairobi mnamo Mei 3 mwaka huu.