Habari MsetoSiasa

Nitakwama na Ruto hata mkinipokonya cheo – Washiali

June 1st, 2020 1 min read

MBUNGE wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali, amekiambia chama cha Jubilee kimuondoe kutoka kwa wadhifa wa Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa iwapo kinataka kufanya hivyo.

Bw Washiali alisema amekuwa akipewa vitisho kuwa akome kushirikiana na Naibu Rais William Ruto la sivyo aondolewe wadhifa huo wake bungeni.

“Niko tayari kuwarejeshea kiti chao ikiwa wanataka kukichukua kwani kuwa Kiranja wa Wengi sio suala la kufa na kupona. Sitapiga magoti mbele ya yeyote kuomba kuendelea kushikilia nafasi hii,” alisema Bw Washiali katika mahojiano na Taifa Leo nyumbani kwake katika kijiji cha Shitoto, Kaunti ya Kakamega.

Alieleza masikitiko kuwa waliopinga kuchaguliwa tena kwa Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2017 sasa wameungana kuvunja Jubilee.

Bunge la Kitaifa linatarajiwa kurejelea vikao vyake kesho huku harakati za kuwaondoa wanaoegemea kwa Dkt Ruto zikiendelea.

Bw Washiali alimtaja Dkt Ruto kama rafiki wa kifamilia kwa muda mrefu, na ambaye wamekuwa wakisaidiana kwa mambo mengi.

Na Shaban Makokha