HabariSiasa

Nitampinga Uhuru akiunga referenda – Kuria

July 21st, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria amesema kuwa yuko tayari kumpinga Rais Uhuru Kenyatta, endapo ataunga mkono kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Kulingana na mbunge huyo, kuandaliwa kwa refarenda wakati huo kutainyima serikali nafasi ya kuendesha maendeleo, na badala yake kuendeleza siasa.

Bw Kuria alisema japo pia naye anaunga mkono kuandaliwa kwa kura ya maamuzi ili mabadiliko fulani ya kikatiba yafanywe, wakati muafaka kwake utakuwa wakati wa uchaguzi wa 2022.

“Siwezi kuunga mkono referenda iandaliwe kabla ya 2022. Naunga mkono hatua ya katiba kufanyiwa marekebisho kadhaa, lakini yale yanawezekana kufanywa na bunge yafanywe sasa, kisha wakati wa Uchaguzi Mkuu 2022 tupige kura ya maamuzi,” Bw Kuria akasema.

“Hatutasimamisha taifa ili kufanya referenda. Haitafanyika hivyo,” akasema.

Alisema hivyo wakati timu ya BBI inaelekea kukamilisha zoezi lake la kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya, huku ikitarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Kumekuwa na matarajio kuwa huenda BBI ikapendekeza referenda iandaliwe, lakini mjadala kuhusu muda ambao inafaa kuandaliwa na masuali yanayofaa kuulizwa umeibua hisia kali.

Kikatiba, kuna baadhi ya mabadiliko ambayo sharti yafanywe na wananchi katika referenda, na pia kuna mengine ambayo yanaweza kufanywa n bunge.

Hata hivyo, referenda ikiandaliwa wakati wa uchaguzi 2022, nchi itaendelea na mfumo wa sasa wa uongozi hadi 2027, ambapo mfumo utakaopitishwa utaanza kazi.

Lakini uamuzi wa mwisho bado utategemea ripoti ambayo BBI itawasilisha, ambao unatarajiwa kutoa maoni ya Wakenya, viongozi na mashirika.