HabariSiasa

Nitamwonyesha Ruto kivumbi 2022 – Joho

July 24th, 2018 2 min read

Na WINNIE ATIENO

Gavana wa Mombasa Hassan Joho amepuzilia mbali ziara nyingi za Naibu Rais katika eneo la Pwani kutafuta kuungwa mkono, katika azma yake ya kuwania urais 2022, akisema yeye bado ndiye jogoo wa mwambao.

Naibu huyo wa kiongozi wa ODM alisema Bw Ruto anapoteza muda wake Pwani na akaapa kumwonyesha kivumbi 2022 kwa kufanya kazi na wapinzani wa Naibu Rais kuhakikisha ameambulia patupu.

Katika siku za majuzi Bw Ruto amenyemelea Pwani mara tisa tangu mwanzoni mwa mwaka huu, na juhudi zake zimezaa matunda kwani amevua wabunge 15, ambao wamemwambia watamfanyia kampeni eneo la Pwani 2022.

Hata hivyo wadadisi wa siasa za Pwani wanasema ni mapema mno kuamua mustakabali wa wakazi wa eneo hilo.

Pia wanadokeza kuwa huenda wabunge hao wasimfae Bw Ruto kwenye uchaguzi wa 2022 ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya wabunge eneo hilo huwa hawachaguliwi kwa awamu mbili.

Kwenye uchaguzi wa 2017 wabunge wengi walikojitambulisha na Serikali walipigwa kumbo na wakazi.

Eneo hilo limekuwa likimuunga mkono kwa dhati kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Bw Joho anapania kutegemea ngome zake kwenye azma yake ya kuwania urais.

Licha ya kampeni za kisiasa zilizoanzishwa mapema Pwani, matatizo mengi ya wenyeji hayajashughulikiwa kwani wangali wanakabiliwa na uhaba wa mashamba, umaskini mkubwa, miundo msingi duni miongoni mwa matatizo mengine chungu tele.

Akiongea jana alipofungua wadi ya kina mama wanaopata changamoto baada ya kujifungua katika Hospitali Kuu ya Pwani, Bw Joho alisema azma yake ya kuwania uongozi wa kitaifa haitasimamishwa na yeyote.

Alisema wale wanaopinga ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga ni viongozi wanaoendeleza siasa za chuki.

“Lazima tushirikiane ili tuwe na amani. Kama si ufisadi Kenya ingekuwa mbali sana, kwani fedha hizo zingetumiwa kuboresha maisha ya Wakenya,” akasema.

Mbunge wa Likoni, Mishi Mboko alimuunga mkono akimpa moyo Bw Joho: “Usibabaishwe Bw Joho tuko nyuma yako na tutakusimamia. Wabunge wanaomfuata Bw Ruto wanafanya hivyo ili kumdhalilisha Bw Joho ilhali ni mpwani mwenzenu. Mujue urais unatoka kwa Mungu wala si binadamu.”

Aliwafokea wanasiasa ambao wanazunguka kila pembe ya nchi wakichapa siasa za 2022 akiwataja kama wasio na ajenda ya kuwafaa wananchi.

“Hawa ni watu waliopoteza mwelekeo. Mwingine anadhania ni tajiri sana kila asemacho Wakenya waamini au wafuate. Lakini Wakenya ni wajanja sana na wanaelewa,” akaeleza Bi Mboko.