Habari

Nitarejea kwa maisha yenu kama pepo, Bob aliwaambia marafiki

July 2nd, 2019 1 min read

NA MARY WANGARI

AFISA Mkuu Mtendaji wa kampuni ya uanahabari ya Radio Africa Group Bw Patrick Quarcoo, amefichua kuwa ombi kuu la aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom Bob Collymore lilikuwa marafiki zake wasimame na mkewe, Wambui Kamiru, baada ya yeye kuipa dunia kisogo.

Katika usimulizi wa kipekee aidha, Bw Quarcoo alikumbuka jinsi katika kikao chao cha mwisho, mkuu huyo wa Safaricom aliyekuwa daima mwingi wa uchangamfu alivyotania katika jinsi angerejea kama pepo.

“Sijui kuhusu jambo hili la mbinguni na duniani, lakini natumaini kwa dhati kwamba kuna uhai baada ya kifo,” alisema Bw Collymore.

“Tulipomuuliza ni kwa nini alitujibu kwa utani, ‘iwapo kuna mapepo, nitarejea na kufungua pazia, na wakati wa sherehe za siku ya kuzaliwa kwa watoto wangu mtakapowasha mishumaa nitakuja na kuwasaidia kuipuliza,’ alisema.

Mzaliwa huyo wa Guyana alikuwa akizungumza na kundi mahsusi la masahibu wake ambao ni pamoja na Quarcoo, Jeff Koinange, Bharat Thakrar, Nic Hailey, Peter Kenneth na Alykhan Satchu.

Katika wosia ulioibua hisia mseto, Bw Quarcoo alisimulia ujumbe wa mwisho wa kigogo huyo kuhusiana na mkewe mpendwa.

“Nikijaliwa kuishi kwa siku tatu zaidi nitakuwa na bahati. Dumisheni umoja, simameni na mke wangu Wambui nikiondoka,”  akasema Bob Collymore katika usemi wake wa mwisho duniani.

Bw Quarcoo alimkumbuka marehemu Collymore kama mtu “aliyewabadilisha marafiki zake wote. Alitufanya kuwa na utu zaidi, wenye moyo safi zaidi kama yeye binafsi na kuwa rahisi kufunguka,”

Bw Collymore aliaga dunia baada ya kulemewa na gonjwa la saratani hapo Julai 1, 2019.