Michezo

Nitatia saini mkataba mpya Man-City nikihisi kwamba nastahili kufanya hivyo – Pep

September 21st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola, 49, amesema atatia saini mkataba mpya kambini mwa Manchester City iwapo atahisi “anastahiki”kufanya hivyo badala ya kupewa tu.

Kandarasi ya sasa kati ya mkufunzi huyo raia wa Uhispania na Man-City unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu na ni matamanio ya usimamizi wa miamba hao kumshuhudia Guardiola akirefusha muda wake ugani Etihad.

Guardiola anaanza msimu wake wa tano kambini mwa Man-City mnamo Septemba 21 atakapowaongoza waajiri wake kuvaana na Wolves katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika uwanja wa Molineux.

Hiki ndicho kipindi kirefu zaidi kwa Guardiola kuhudumu katika kikosi kimoja baada ya kudhibiti mikoba ya Barcelona (2008-12) na Bayern Munich (2013-16).

“Ningependa sana kusalia hapa Etihad kuwanoa Man-City. Nimeishia kuyapenda mazingira ya hapa ila nahitaji kustahili kupewa kandarasi mpya. Man-City wamefaulu kujivunia mengi katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita na ni lazima tuendeleze rekodi hiyo,” akasema Guardiola ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Barcelona.

Kwa mujibu wa Guardiola, hakuna yeyote kati ya Mwenyekiti Khaldoon Al Mubarak au Afisa Mkuu Mtendaji Ferran Soriano ambaye amewahi kumzungumzia kuhusu mkataba mpya.

Ingawa hivyo, anahisi kwamba matarajio kutoka kwake ni ya kiwango cha juu hasa baada ya kusuasua kwao muhula uliopita ambao ulishuhudia pengo la alama 18 likitamalaki kati yao na mabingwa Liverpool.

Isitoshe, Man-City walibanduliwa na Olympique Lyon ya Ufaransa kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na hilo likawapa Bayern kibarua chepesi cha kudengua Lyon (3-0) kwenye nusu-fainali na hatimaye kutwaa ufalme baada ya kuwapiga Paris Saint-Germain (PSG) 1-0 kwenye fainali jijini Lisbon, Ureno.

“Wasimamizi wa Man-City hawakunipa masharti: kwamba lazima utimize haya au yale ndipo urefushiwe kandarasi. Waliniambia niongoze kikosi kucheza soka nzuri,” akatanguliza.

“Lakini najua hadhi ya klabu hii pamoja na matamanio yao. Matarajio kutoka kwa mashabiki pia ni ya kiwango cha juu. Lazima turejelee kushinda mataji,” akaongeza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO