HabariSiasa

Nitatoa ushahidi tume ya kuchunguza kifo cha Msando ikiundwa – Akombe

August 3rd, 2020 2 min read

Na PATRICK LAGAT

KIFO tatanishi cha aliyekuwa mkuu wa kitengo cha teknolojia katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) marehemu Chris Msando, kinaendelea kuzua mgawanyiko huku wito ukitolewa kubuniwe kwa tume ya kuchunguza mauti yake.

Bw Msando aliuawa kinyama na mwili wake kutupwa katika kichaka kimoja eneo la Kikuyu siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.Aliyekuwa kamishina wa IEBC, Dkt Roselyne Akombe, ametoa wito kuundwe tume ili kubaini ukweli kuhusu kifo cha Bw Msando, akiahidi kwamba atakuwa tayari kutoa ushahidi kwenye tume hiyo.

“Mnamo Julai 29, nilisema nitatoa ushahidi iwapo tume huru itaundwa kuchunguza mauaji ya mwenzangu Chris,” Dkt Akombe akaandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Baada ya kuandika hayo, Dkt Akombe alisema kwamba alipokea barua pepe kutoka kwa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Bw Ezra Chiloba akikanusha madai yake.

“Roselyne, usijaribu kuandika upya historia. Kimya chetu si leseni yako. Wako Chiloba,” akaandika Bw Chiloba kwenye mazungumzo na Dkt Akombe.

Ni jibu la Bw Chiloba ambalo lilimsukuma Dkt Akombe kuwataka Wakenya waelezwe ukweli kuhusu mauti ya marehemu Bw Msando.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu mazungumzo hayo, Bi Akombe alikataa kujibu akisema ‘Siwezi kusema chochote. Wakenya wanahitaji kufahamu ukweli. Jibu la Bw Chiloba linathibitisha kwamba tume ya uchunguzi inafaa kuundwa,” akasema Dkt Akombe.

“Mnamo 2013 teknolojia haikufeli. Watu ndio walifeli teknolojia,” alisema marehemu Bw Msando wakati wa hafla ya kuangazia kujiandaa kwa IEBC kusimamia uchaguzi mnamo Juni 12.

Hii ilikuwa miezi miwili kabla hajauawa kikatili. Bw Msando anakumbukwa kwa kusema kuwa uchaguzi nchini Kenya huwa ghali kwa sababu watu huwa hawaaminiani.

“Hatuaminiani ndiyo maana Wakenya hutumia mabilioni ya fedha kufidia kutoaminiana,’ akasema kwenye mahojiano kadhaa na Taifa Leo wiki chache kabla ya mauti yake.

Kupitia twitter na ikiwa miaka mitatu tangu marehemu Bw Msando auawe kinyama, Dkt Akombe alidai kwamba baadhi ya wafanyakazi wenzake walihusika kwenye mpango mzima wa kumuua mwenzao.

“Siku kama hii miaka mitatu iliyopita, wafanyakazi wenzako walikuongoza kwenye mauti. Kama Yuda, walikuuza kwa mapeni 30 pekee. Hatimaye tutapata haki kuhusu kifo chako kilichojaa uchungu hata ikichukua muda gani,” akaandika Dkt Akombe.

Hapo jana, Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati hakujibu ujumbe au simu zetu ila alinukuliwa wiki jana na gazeti la The Star akisema kwamba bado wanatafuta haki wakilenga kujua kilichomuua Bw Msando.

“Inaonekana kuna jambo analolifahamu ambalo sisi hatulijui. Naamini kwamba anafaa kutoa habari hizo kwa vitengo vya uchunguzi. Maelezo yake yatasaidia kukamilisha uchunguzi,” akasema Bw Chebukati.

Tangu ajiuzulu kutoka IEBC siku chache kabla ya marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26, 2017, Dkt Akombe amekuwa akikosoa utendakazi wa tume hiyo.

Kabla ya kuteuliwa kamishina mnamo 2017, Dkt Akombe aliacha kazi yake yenye mapato mazuri katika Shirika la Umoja wa Kimataifa (UN).