Siasa

Nitaunda chama changu cha kisiasa, Mwadime amwambia Raila

January 27th, 2024 2 min read

NA LUCY MKANYIKA 

GAVANA wa Kaunti ya Taita Taveta Andrew Mwadime amesema kuwa ataunda chama chake cha kisiasa ambapo yeye atakuwa kinara.

Akiongea wakati wa mkutano wa wajumbe wa Orange Denocratic Movement (ODM) uliofanyika katika hoteli ya Panlis, Mwatate, gavana Mwadime alisema ataanzisha chama chake baada ya msukosuko aliokabiliana nao katika mchujo kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Mkutano huo ulihudhuriwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga na viongozi wengine wa chama hicho, wakiwemo Naibu Mwenyekiti Wycliffe Oparanya, Katibu Mkuu Edwin Sifuna, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir, Seneta wa Taita Taveta Jones Mwaruma na viongozi wengine.

Bw Mwadime aliambia Bw Odinga kuwa atafanya majadiliano naye kuhusu wazo hilo lake, akisema kuwa uamuzi utaafikiwa baada ya hapo.

Bw Mwadime alichaguliwa kupitia tiketi ya mgombea huru wa kujitegemea baada ya juhudi zake za kupata bendera ya ODM wakati wa uchaguzi uliopita kugonga mwamba.

“Nilikuwa na matatizo na chama cha ODM na hiyo ikasababisha mimi kuwa mgombea huru. Lakini nitakuja kwako tujadiliane kwa kuwa nataka kuwa kinara wa chama na kuwa kinara lazima tuwe na chama cha Mwadime,” akasema.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga (kushoto) akiwa na Gavana Andrew Mwadime (kati) na diwani maalum wa ODM Hope Anisa katika hoteli ya Panlis mjini Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta. PICHA | LUCY MKANYIKA

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wakiwemo Bw Oparanya na Bw Mwaruma walisema kuwa viongozi wasioegemea mrengo wowote wa kisiasa hawana ushawishi wowote wa kutetea maslahi ya wananchi.

“Msipigie viongozi wanaosimama kama wagombea huru. Wao ni kama popo, si ndege si mnyama. Ifikapo uchaguzi ujao tuchague viongozi wa chama cha ODM,” akasema Bw Mwaruma.

Bw Oparanya alisema kuwa chama cha ODM ni chama cha kitaifa na kina wafuasi wengi katika kaunti ya Taita Taveta na maeneo mengine ya nchi.

Alisema kuwa kubuniwa kwa vyama vidogo havinufaishi wenyeji na kutoa mfano wa chama cha PAA ambapo hivi majuzi baadhi ya viongozi wake walihamia ODM.

“Wakati wa uchaguzi vyama vingi vidogovidogo hujitokeza. Wanasema kuwa wanataka chama chao cha kutetea maswala yao. Wale wanaofanya hivyo wanajitafutia maswala yao wenyewe kwa hivyo mjihadhari na watu kama hao,” alisema.

Bw Oparanya aliwataka wenyeji wa eneo hilo kukatalia katika chama cha ODM na wale hawajajisajili wajiunge wakati wa shughuli hiyo inayoendelea.

Waliwataka wenyeji kujiandikisha kwa wingi kwa chama hicho na kushiriki katika shughuli zake.

Hapo Ijumaa ilikuwa mara ya kwanza kwa kinara huyo kutembelea kaunti hiyo tangu uchaguzi uliopita.

Katika uchaguzi uliopita, chama hicho kilipoteza nyadhfa nyingi za kisiasa na kuibuka na ushindi wa useneta na wawakilishi tano pekee wa bunge la kaunti kinyume na chaguzi za hapo awali.

Aidha, miaka ya nyuma Bw Odinga alikuwa akipokea uungwaji mkono mkubwa na magavana wa zamani wakiwemo John Mruttu aliyekuwa amechaguliwa na tiketi ya ODM katika uchaguzi wa 2013 na mrithi wake Granton Samboja ambaye alichaguliwa na chama cha Wiper.

Alipokuwa mamlakani, Bw Samboja alionekana kumshabikia Bw Odinga kwa kiasi kikubwa kuliko kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.