Habari Mseto

Nitaunga mkono muafaka UhuRuto wakiomba radhi kwa kuiba kura – Miguna

September 26th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKILI mbishi Dkt Miguna Miguna ameapa kuwa hawezi kukubali muafaka wowote na viongozi wa serikali ya Kenya hadi wakubali kuwa waliiba kura kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Dkt Miguna, aliyefurushwa Kenya kwa madai ya kukosa stakabadhi halali za uraia, alisema kwamba hawezi kuunga wito wa upatanishi nchini iwapo Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Wake William Ruto hawatakiri hadharani kwamba waliiba kura na kuomba msamaha.

Wakili huyo anaonekana kuwa mtu wa pekee anayezungumzia suala la haki katika uchaguzi baada ya muafaka wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

“Siku ambayo @UKenyatta na @WilliamsRuto wataomba msamaha hadharani kwa kuiba kura, kukubali uchunguzi huru wa sava za @IEBCKenyandiyo nitaunga juhudi zao,” Bw Miguna anayeishi Canada aliandika kwenye Twitter.

Wakili huyo alikataa wito wa serikali wa kuhalalisha uraia wake Kenya akisema hakuukana alipopata uraia wa Canada.

Amekuwa akisisitiza kuwa yeye ni raia wa kuzaliwa nchini Kenya na kwamba serikali imekuwa ikikadamiza haki zake.

Alijipata matatani baada ya kuongoza hafla ya kumuapisha Raila Odinga kuwa “rais wa wananchi” mnamo Januari 30 katika bustani Uhuru Park.

Raila alipatana na Rais Kenyatta na wakazika tofauti zao na kuanza juhudi za kuunganisha Wakenya.

Bw Miguna amekuwa akipinga muafaka huo akidai Raila alilipwa na Rais Kenyatta ili kuacha kupinga serikali yake na kutetea Wakenya.

“ Msikubali kupotoshwa kwa zoezi la uhusiano mwema. Enezeni ukweli. Hakuna kiwango cha propaganda kitazuia mageuzi. Msiogope kueneza ukweli. Sambaratisheni uongo unaoenezwa,” aliandika Bw Miguna

Mwezi jana, alitangaza kuwa angerejea nchini baada ya Septemba 24 licha ya kukataa kutuma maombi ya kuhalalisha uraia wake Kenya.