Habari za Kitaifa

Nitawafichua wanaotudai na kuweka wazi kiasi cha pesa tunazodaiwa, Mbadi aahidi


TAARIFA zote za deni la taifa zitawekwa hadharani ikiwa bunge litaidhinisha John Mbadi kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi.

Bw Mbadi ameambia Kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu uteuzi kwamba akiidhinishwa, Wakenya watajua wanadaiwa na nani na kwa kiasi gani.

Kwa mujibu wa mbunge huyo wa kuteuliwa, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wake katika kushughulikia suala la deni kubwa la umma linaloendelea kusakama nchi.

“Ikiwa Wakenya wanadaiwa pesa, kwa nini watu hawajui na ni kiasi kipi kwa sababu si serikali au hazina inayowadai, ni watu wa Kenya,” Bw Mbadi alisema.

Bw Mbadi aliambia kamati hiyo inayoongozwa na Moses Wetang’ula kwamba mabilioni yanayokopwa na serikali kila mara yamekuwa yakiwekwa siri na kuwaacha Wakenya wengi wakihoji ni kiasi gani cha pesa Kenya inadaiwa.

“Ni mikataba gani hii ya siri inayotuzuia kujua tunadaiwa na nani na kwa kiwango kipi? Wakenya wanapaswa kujua wanadaiwa na nani na kwa kiasi gani. Nitaliweka hadharani jambo hili,” Bw Mbadi aliambia Kamati.

Alisema kutokana na kukosekana kwa uwazi katika madeni hayo, mabilioni yanayokopwa kamwe hayatumiki kwa malengo yaliyokusudiwa, hivyo kusababisha Wakenya kulipia kile ambacho hawakufaidika nacho.

“Uwajibikaji wa deni ndilo jambo ambalo watu wengi wanataka. Ukiwasikiliza Wakenya wanauliza deni letu ni la kiasi gani hasa! Hiki ndicho kitu nitakipa kipaumbele iwapo Bunge hili litaniidhinisha,” Bw Mbadi alisema.

Bw Mbadi aliongeza kuwa, kuna haja ya kupunguza ukopaji na kuunganisha pesa zinazokopwa na miradi mahsusi hivyo basi kupunguza hasara.

“Lazima tufanye kazi ya kuunganisha miradi na mikopo. Hatuwezi kukopa ili kufadhili bajeti yetu au kufadhili mambo mengine ambayo si ya maendeleo, nchi inakopa bila pesa kwenda kwa miradi mahsusi,” Bw Mbadi alisema.

Kuhusu kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 na jinsi atakavyokusanya pesa za kuendesha nchi, Bw Mbadi aliwaambia wabunge kwamba kulikuwa na vipengele vizuri katika mswada huo uliokataliwa ambavyo ananuia kuwasilisha kama marekebisho ya mswada wenyewe.

Alisema mswada uliokataliwa haukufafanuliwa ipasavyo kwa Wakenya, jambo lililosababisha wananchi kuupinga.

“Kuna vifungu ambavyo havina ubishi katika mswada huu (wa Fedha ulioondolewa), ambavyo bado vinaweza kusaidia Kenya. Tunaweza kuleta marekebisho mahsusi kwa sheria hizo kwa kushirikisha umma ipasavyo. Umma ulisema haukushirikishwa ipasavyo, jambo ambalo lilifanywa, lakini pengine watu waliona hawakusikilizwa. Mswada huo ukawa mbaya machoni pa umma na ikabidi ukataliwe kwa jumla kwa sababu ya ukosefu wa mawasiliano ya wazi,” Bw Mbadi alisema.

Pia alieleza kuwa Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) inahitaji kufanyiwa mageuzi ili kuipa uwezo muhimu wa kukusanya ushuru zaidi.

Bw Mbadi alidokeza kuwa mifumo ya sasa inayotumiwa na KRA ni mibovu na imechangia ufujaji wa ushuru unaofikia mabilioni ya pesa na jambo hilo linaathiri mapato ya nchi.

“Suluhisho la kukusanya ushuru katika nchi hii ni kulenga KRA, mfumo wao unahitaji kuundwa upya, tunapoteza pesa nyingi kupitia magendo kwa sababu hatuna mfumo mzuri,” akaeleza.