Habari MsetoSiasa

Niteue niwe naibu wako, Passaris amrai Sonko

June 5th, 2018 1 min read

Na COLLINS OMULO

MWAKILISHI wa Wanawake katika Kaunti ya Nairobi Esther Passaris, ametangaza kwamba angetaka kuwa naibu gavana mpya wa kaunti hiyo.

Bi Passaris alisema kwamba yuko tayari kujiuzulu kama Mwakilishi wa Wanawake ili kujaza nafasi hiyo ambayo iliachwa wazi baada ya aliyekuwa naibu gavana Polycarp Igathe kujiuzulu mnamo Januari.

Bi Passaris alisema kuwa azma yake inawiana na mwafaka wa kisiasa uliofikiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Nimemwomba Gavana Mike Sonko aniteue kama naibu wake. Bw Sonko anahitaji naibu ili kuimarisha uongozi wa jiji. Ikiwa bado hajapata, niko tayari kuchukua nafasi hiyo, kwa msingi wa mwafaka huo. Hili litatuwezesha kuimarisha ushirikiano kati ya Jubilee na Nasa katika uongozi wa Nairobi,” akasema Bw Passaris.

Aidha, alisema kwamba yuko tayari kuchukua nafasi hiyo ikizingatiwa kwamba Bw Miguna Miguna amekataa kuukubali, baada ya kuteuliwa na Bw Sonko mwezi uliopita.

Kiongozi huyo alisema kuwa wakazi wa Nairobi wanateseka sana kwa kukosa naibu gavana. Alisema kwamba Bw Sonko ana majukumu mengi sana ambayo hawezi kuyatimiza akiwa peke yake.

“Ikiwa hatutashughulikia hali ya umaskini katika jiji hili, basi utoaji wa huduma nyingine muhimu utakumbwa na changamoto chungu nzima. Watu wengi wametamaushwa na ombwe la uongozi lililopo,” akasema kiongozi huyo.

Kiasi cha pesa kinachotengewa Mwakilishi wa Wanawake ni kidogo sana kushughulikia matatizo mengi yanayowakumba wakazi,” akasema.

Hata hivyo, alitoa sharti kwamba lazima aelezwe kiwazi majukumu ambayo atakuwa akitatekeleza. Alisema kuwa anapaswa kupewa angaa idara tatu muhimu kusimamia ili kuimarisha utoaji huduma.

“Anahitaji mtu kama mimi aliye na tajriba kubwa ya uongozi. Hata hivyo, nitakubali uteuzi tu ikiwa nitaelezwa majukumu nitakayotekeleza,” akasema.