Habari

NJAA: Chifu matatani kwa kufichua vifo

March 20th, 2019 2 min read

FLORAH KOECH, PETER MBURU Na FAITH NYAMAI

CHIFU mmoja katika Kaunti ya Baringo amejipata matatani kwa kuwafichulia wanahabari kuwa wakazi wamekufa kutokana na njaa, huku ikiripotiwa kuwa zaidi ya watu 17 wameangamia.

Chifu wa Kositei, Bw Jackson Ronei na diwani wa wadi ya Kositei, Bw Daniel Tuwit, wametakiwa wafike ofisi ya utawala wa kaunti kuandikisha taarifa kuhusiana na habari walizotoa kwa wanahabari kuhusu athari za njaa eneo hilo.

Serikali imekanusha kuwa kuna watu waliokufa kutokana na njaa huku Afisa Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Kiangazi (NDMA), James Oduor akisema waliokufa walikuwa wagonjwa.

Kauli hiyo ilirudiwa jana na Mshirikishi wa Serikali eneo la Rift Valley, Bw Mwongo Chimwaga, aliyesisitiza kuwa hakuna watu waliokufa kutokana na njaa.

“Hakuna hata mtu mmoja aliyekufa Baringo na Turkana kama ilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari,” akasema Bw Chimwaga.

Lakini msimamo huo ulipingwa jana wakati wa kusambaza chakula cha msaada katika eneo la Nginyang’, Kaunti ya Baringo pale diwani wa Silale, Bw Nelson Lotela, alipomwambia Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa kuwa ana orodha ya zaidi ya watu 17 waliokufa kwa maradhi yanayotokana na njaa.

“Nashangaa kwa nini serikali inakanusha habari za watu kufa kwa njaa, ilhali sisi watu wa mashinani tuna ushahidi kuwa watu wanakufa kwa njaa? Mzee Kisera Apewot alikufa Jumatatu jioni nyumbani mwake baada ya kukaa njaa kwa siku kadhaa,” akasema Bw Lotela.

Wanahabari ambao wamezuru maeneo yanayoathirika wamesisitiza kuwa hali ni mbaya hasa Baringo na Turkana.

Jijini Nairobi, Bunge lililazimika kutenga muda kujadili janga la njaa nchini baada ya Spika Justin Muturi kukubali ombi la mbunge wa Ndhiwa, Martin Owino.

Mnamo Jumatatu, Serikali ilitoa Sh2 bilioni za kuwalisha Wakenya wanaokabiliwa na njaa maeneo yaliyoathiriwa.

Kiasi hicho ni cha chini ikilinganishwa na Sh6 bilioni ambazo Wizara ya Ugatuzi ilikuwa imeomba kuwezesha kutolewa kwa chakula cha msaada kwa wakazi hasa katika kaunti za Turkana, Baringo, Samburu, Marsabit, Mandera, Wajir na Garissa. Zingine ni Isiolo, Kilifi, Tana River, Pokot Magharibi, Makueni, Kajiado na Kwale.

Wakati huo huo, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, imetangaza kuwa ukame unaoendelea kushuhudiwa Kaskazini na Mashariki mwa Kenya utaendelea.

Kaimu Mkurugenzi wa idara hiyo, Stella Aura jana alisema hali hiyo itasababisha ukosefu wa maji huku jamii za wafugaji zikipata taabu zaidi kwa kukosa lishe na maji.

Hali hiyo huenda ikachochea mizozo kati ya jamii za wafugaji waking’ang’ania malisho na maji, na pia kati ya wanyamapori na binadamu.