Njaa ilivyouza magaidi

Njaa ilivyouza magaidi

Na BERNARD MWINZI

MAGAIDI watatu walionaswa kichakani katika kijiji cha Kamuluyuni kilichoko eneo la Nuu, Mwingi, Kaunti ya Kitui, baada ya kutoroka kutoka gereza la Kamati, walijaribu kuhonga polisi wa akiba waliowafumania mafichoni.

Uchunguzi wa Taifa Leo, pia umebaini kuwa magaidi hao; Musharaf Abdallah Akhuluya, Joseph Juma Odhiambo na Mohamed Ali Abikar, walihonga walinzi wa gereza la Kamiti wakafunguliwa lango kuu.

Magaidi hao walikamatwa Alhamisi walipokuwa wakipumzika kijijini humo baada ya kutembea umbali mrefu kutoka Gereza la Kamiti, wakapitia Kaunti ya Machakos na kisha kufululiza hadi Kitui.

Watatu hao walilenga kuingia kwenye msitu ulio karibu na mji mdogo wa Endau.

Msitu huo umetanda hadi katika mpaka wa Kenya na Somalia.

Walipofika katika eneo la Kamuluyuni, simu waliyokuwa nayo iliishiwa moto na walilemewa uchovu na makali ya njaa.

Jumatano jioni, Bw Petero Komu Kilonzi ambaye ni polisi wa akiba katika eneo hilo, alipashwa habari na wakazi wa eneo hilo kwamba, waliona watu waliowashuku wakitembea kati ya Kamuluyuni na msitu wa Endau.

Bw Kilonzi alichukua walinzi wenzake na kufufuliza hadi Endao kujionea kilichokuwa kikiendelea katika msitu huo.

Bw Kilonzi, 45, alitwika majukumu ya kuwa polisi wa akiba (APR) mnamo 2017.

“Tuliwatafuta msituni humo usiku mzima lakini hatukuwaona. Ilipofika alfajiri, tulirudi nyumbani kwenda kupumzika,” Bw Kilonzi aliambia Taifa Leo.

Alhamisi asubuhi, Bw Kilonzi na wenzake 15 walirudi msituni lakini ilipofika saa nne asubuhi, walirudi katika eneo la Kamuluyuni.

Polisi wa akiba Bw Petero Komu Kilonzi (kati) akiwa na wenzake waliomsaidia kunasa magaidi waliotoroka Gereza la Kamiti. PICHA | SILA KIPLAGAT

Walipowasili katika soko la Kamuluyuni, Bw Kilonzi aliabiri pikipiki yake na kuzunguka kijijini hapo akiuliza wakazi iwapo walikuwa wamewaona watu waliowashuku.

Afisa huyo wa APR alikutana na mwanamke aliyemwambia kwamba, aliona mwanamume aliyekuja nyumbani kwake kuomba chakula.

Mwanamke huyo alisema kuwa alimpakulia githeri alichobeba na kumpelekea mwenzake aliyekuwa amejificha nyuma ya ua.

Huku wakiendelea na mazungumzo, Bw Kilonzi aliona mtu amejificha kichakani. Bw Kilonzi alimwendea mwanamume huyo ambaye baadaye ilibainika kwamba alikuwa Musharaf Abdalla Akhulunga, aliyehukumiwa kifungo baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kulipua majengo ya Bunge mnamo 2012.

“Nilimsalimia nikamuuliza ikiwa alihitaji usaidizi. Aliniambia kwamba alikuwa muuzaji wa makaa na akanisihi nimsaidie kufika katika eneo la Ukasi. Vilevile, alinieleza kwamba alikuwa na kiu na kunitaka kumsaidia kupata maji,” akaeleza Bw Kilonzi.

Ukasi ni mji mdogo ulioko barabarani kati ya Mwingi na Garissa.

Huku wakiendelea kuzungumza, Bw Kilonzi ghafla alimrukia na kujaribu kumfunga pingu. Lakini Musharaf alikwepa na kuanza kumshambulia Bw Kilonzi.

Baada ya kupambana kwa muda, Bw Kilonzi alimlemea gaidi huyo na kumfunga pingu. Baadaye, Bw Kilonzi pamoja na watu waliofika kumsaidia, walimbeba gaidi huyo na kumweka juu ya pikipiki na kisha kumpeleka katika eneo la soko.

Musharaf alipofika huko, aliomba maji na chakula. Bw Kilonzi alimnunulia chapati na maharagwe.

“Baada ya kushiba, alitueleza kwamba wenzake; Joseph Juma Odhiambo na Mohamed Ali Abikar walikuwa karibu na kutuhakikishia kwamba hawakuwa na nguvu za kuhepa kutokana na uchovu na makali ya njaa,” akasema.

Baadhi ya maafisa wa APR walikimbia msituni na baada ya muda mfupi, waliwanasa Abikar na Odhiambo.

Waliwaketisha karibu na Musharaf na kuanza kuwahoji.

Abikar alianza kupiga mayowe huku akiwasihi maafisa hao wa APR wawaue kwa risasi kuliko kuwarejesha gerezani Kamiti.

Abikar alihukumiwa kifungo baada ya kupatikana hatia ya kuhusika na shambulio la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa ambapo watu 148 waliuawa mnamo 2014.

Alihukumiwa kifungo cha miaka 41 gerezani.

“Alitwambia kuwa alipoteza simu yake msituni tulipokuwa tukimkimbiza na endapo tungemsaidia kuipata angewasiliana na wenzake (bila kutaja walikokuwa) watupatie hongo ya fedha nyingi,” akasema Bw Joseph Kilunda Muthoka, mmoja wa maafisa wa APR.

Abikar aliwataka maafisa wa APR wakubali kuchukua hongo ili wawaachilie huru.

Maafisa wa APR waliwasiliana na polisi wa Kituo cha Nuu ambao walifika katika eneo hilo baada ya muda mfupi.

Odhiambo aliyefungwa kwa kujaribu kujiunga na kundi la wapiganaji la al-Shabaab mnamo 2019, hakutamka neno wakati huo wote.

Walipofikishwa katika Kituo cha Polisi cha Nuu, Abikar alikiri kwamba hawakupanda ukutani kama ilivyodaiwa.

Alifichua kuwa walifunguliwa lango kuu na walinzi wa gereza wakaondoka.

Maafisa wakuu wa gereza la Kamiti tayari wamekamatwa na wanatarajiwa kufunguliwa mashtaka Jumatatu.

  • Tags

You can share this post!

Buffa Otieno abwaga Tundo kuwa mwanamichezo bora nchini wa...

Mamilioni ya Ruto yawasha moto sehemu tofauti nchini

T L