Makala

Njaa inavyoweka kina mama na wasichana kwenye hatari ya dhuluma

February 12th, 2024 3 min read

NA OSCAR KAKAI

BAA la njaa limewaweka akina mama na wasichana wengi katika maeneo kame ya wafugaji kwenye hatari ya maovu ya dhuluma za kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za mapema.

Kutokana na kiangazi ambacho kimeshamiri eneo hilo pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi, akina mama na wasichana wanakabiliwa na ongezeko la maovu hayo.

Uhaba wa chakula kutokana na bei ya juu ya vyakula, inaweka wasichana wadogo kwenye hatari ya kuacha shule, kuolewa wakiwa na umri mdogo na kutumiwa vibaya kingono.

Shirika la Pokot Outreach Ministries (POM) pamoja na machifu wa eneo hilo, wameripoti tishio la maovu hayo huku wasichana wadogo wakiondolewa shuleni na kujiunga na familia zao ambazo huhamahama kutafuta chakula, maji na nyasi za mifugo wao.

Ongezeko la visa hivyo inatokana na gharama ya juu ya maisha na hali ya uchumi kudorora na kufanya maisha kuwa magumu  na kuwafanya wakazi kutegemea maovu hayo ili wajipatie mapato.

Kulingana na machifu hao, hali hiyo imekuwa changamoto kuu kwa kukomesha maovu hayo ambayo yalipitwa na wakati dhidi ya wasichana wadogo ambao kulazimishwa kukeketewa ili kuokoa familia zao kutokana na njaa ambayo huletwa na visa vya utovu wa usalama hali ambayo hufanya wakazi kukosa kuwa na makao kamili.

Haya yalifichuliwa kwenye mkutano wa hamasisho dhidi ya ukeketaji eneo la Orwa.

Chifu wa Lokesheni ya Sekerr, Charles Chepushen, anaeleza kuwa kizingiti kikubwa eneo hilo ni baa la njaa na uhaba wa maji akiongeza kuwa maovu hayo ambayo yalipitwa na wakati hufanyika kutokana na umaskini, ujinga na utovu wa usalama.

“Wakazi ni wafugaji wa kuhamahama ambao hutembea kusaka nyasi, maji na chakula. Mifugo huuawa ana wengine kuibiwa na sasa familia hazijiwezi na wasichana ndio sululu,” alisema.

Anasema kuwa wameweka mikakati ya kukomesha ukeketaji kwa kuwashika wahusika.

 “Tulishika wazazi na wasichana lakini mkeketaji alitoroka. Watu wengi hutumia njia za mkato kuoza wasichana wao ili kupata mahari ili wapate chakula,” anasema.

Florence Mondi, afisa wa kusimamia masuala ya akina mama katika shirika la POM anasema kuwa ukeketaji una athari mbaya kwa afya ya akili ya wasichana na akina mama na maisha yao kwa ujumla na yanafaa kulindwa.

“Wasichana huozwa kwa wazee ambao wako na mali. Msichana kifungua mimba na wa pili huwa wanaozwa. Wanajua ni warembo na wataleta ng’ombe wengi. Tunafaa kusikiza sauti zao ili wapate elimu wawe viongozi na kusaidia watu wengine,” alisema.

Alisema kuwa utovu wa usalama huchangia baa la njaa katika eneo hilo.

“Wakazi hukosa njia mbadala za kujikimu baada ya mifugo wao kuibiwa. Waliokuwa wezi wa mifugo na kuasi hutegemea kazi na ikiwa kazi hiyo inasimama wakakosa cha kuwapatia riziki na huwa na changamoto nyingi kupata chakula,” anasema.

Anasema kuwa wanaume ndio wanachangia wasichana wadogo kuozwa.

“Wanaoa wasichana wenye umri wa miaka 12. Unaweza kupewa mahari ya ng’ombe 50 lakini zinaibiwa ama ugonjwa unawaua. Usiangalie utajiri wa sasa bali muelimishe wasichana ambao watakuwa matajiri siku za usoni,” anasema.

Seneta wa Kaunti ya Pokot Magharibi Julius Murgor alisema kuwa wazazi wanafaa kukumbatia elimu akisema kuwa kiangazi kwa miaka 40 kimekuwa kikisukuma familia pabaya na kuweka wasichana wanaobalehe kwenye hatari.

“Familia huwa na chaguo mbovu kujikimu wakati wa kiangazi kutokana na mabadiliko ya hali ya anga, hukausha chemichemi za maji na kuuawa kwa mifugo. Idadi kubwa ya wazazi na walezi wanawaoza wasichana kupata mahari ili walishe familia pana,”alisema.

Seneta Murgor anasema kuwa visa vya ndoa za mapema na ukeketaji vinawasukuma wasichana wadogo kuondoka shuleni na kuwaacha na dhuluma za kijinsia nyumbani na umasikini wa miaka na mikaka.

“Tunashuhudia tishio la ongezeko la ndoa za watoto na ukeketaji katika eneo hili ambapo familia nyingi za uchochole zinapanga kuwaoza wasichana wenye umri wa miaka 12, kwa wazee wenye umri mara tano kuwaliko,” anasema Kasisi Murgor.

Anasema kuwa katika eneo hilo kame, akina mama na wasichana hutembea mwendo mrefu kupata maji na mahitaji mengine na kuwaacha kwenye hatari ya dhuluma za kingono.

“Akina mama na wasichana kutembea kwa zaidi ya kilomita 30,” alisema.

Alisema kuwa ukeketaji huleta hatari za kiafya kama kuzimia, uchugu mkubwa, maambukizi ya bakteria ambayo huajiri afya ya akili ya akina mama na hata wengine kuaga dunia.

Mwakilishi wa wadi ya Sekerr Jane Mengich alisema kuwa masomo ya wasichana hukatizwa na matumaini na ndoto zao kuzima.

“Wengi huwa katika hali mbaya na kuacha shule kisha wanajiingiza kwenye shida ili wapate chakula. Maisha ya wengi huharibika baada ya kuwa washerati,” alisema Bi Mengich.

“Wakati wa kiangazi, akina mama na wasichana ndio huathirika sababu hupanga foleni kutafuta maji,” aliongeza kusema.

[email protected]