Habari

Njaa kuu yaja

January 30th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

JANGA la njaa linakodolea Wakenya macho kufuatia uvamizi wa nzige ambao wanaendelea kusababisha uharibifu mkubwa wa mimea nchini.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo duniani (FAO) ambalo husimamiwa na Umoja wa Mataifa (UN), nzige waliokomaa na wengine wachanga walikuwa wameonekana katika kaunti 13 kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kufikia Jumatano, wadudu hao waharibifu waliendelea kuenea maeneo mengi nchini.

Serikali sasa imekiri hali hii itasababisha ugumu wa hali ya maisha mwaka 2020 kutokana na athari mbaya kwa kilimo na uchumi.

Kwenye taarifa ya sera ya bajeti ya mwaka wa 2020/2021, Waziri wa Fedha Ukur Yatani alisema, athari ya nzige kwa kilimo itasababisha gharama ya maisha kupanda na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi.

“Uvamizi wa nzige nchini mwishoni mwa 2019 hadi mapema 2020 ni hatari kwa kilimo na uzalishaji wa chakula cha kutosheleza mahitaji ya wananchi. Serikali itaendelea kufuatilia hali hiyo na kuweka mikakati ya kifedha na sera za kuimarisha uchumi,” akasema.

Janga la nzige kama la sasa halijashuhudiwa nchini kwa miaka 70.

Wakulima katika maeneo yanayosifika kwa uzalishaji wa chakula ya Rift Valley na magharibi mwa nchi wana matumaini kwamba ushauri wa wataalamu wanaosema upepo hautawaruhusu nzige kuelekea huko utakuwa wa kweli.

Sehemu nyingi za nchi ambazo zimevamiwa kufikia sasa ni maeneo ambapo wananchi hutegemea ufugaji kujipatia. Hali hii inaibua hofu ya vita vya kijamii kwa wafugaji watakaokosa malisho ya mifugo wao siku zijazo.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Bw QU Dongyu, alisisitiza ni sharti hatua zote zinazochukuliwa zijumuishe juhudi za kuwezesha wakazi kukidhi mahitaji yao ili kuzuia athari zaidi.

“Jamii za Afrika Mashariki tayari hukabiliwa na ukame wa muda mrefu ambao umeathiri uwezo wao wa kilimo na riziki. Tunahitaji kuwasaidia kurudia hali yao ya kawaida pundenzige watakapoondoka,” akasema.

Kwa mujibu wa mwongozo wa UN kuhusu mbinu za kupambana na ghasia za kupigania rasilimali, uhaba au ukosefu wa mali asili zinazotegemewa na binadamu kama vile lishe ya mifugo na maji huwa ni mojawapo ya sababu kuu za vita vya kijamii.

Takwimu zinaonyesha kuwa, wingu moja la nzige huweza kutafuna takriban kilo milioni 192 ya mimea kwa siku. Uzani huu ni sawa na takriban magunia milioni mbili ya mahindi ya kilo tisini kila moja.

Imebainika kwamba, wakati nzige wanavamia eneo, masomo huathirika kwa kuwa watoto hutolewa madarasani kwenda kuwashtua watoroke.

Mnamo Jumanne, hali hii ilishuhudiwa katika eneo la Masaku, Kaunti ya Machakos ambapo mamia ya wanafunzi wa shule za msingi na upili waliungana na walimu na wazazi kwa takriban saa 15 kufukuza nzige.

Mbinu ya kunyunyiza dawa kutoka angani kuua nzige pia inaibua hofu ya uharibifu wa mazingira na athari za kiafya.

Ingawa serikali na asasi nyingine zinazohusika katika shughuli hiyo zilihakikishia umma kuhusu usalama wa kemikali zinazotumiwa, ripoti zinasema si rahisi kuepuka athari kwa afya na mazingira hasa nzige wanapoongezeka na kufanya dawa nyingi zaidi kumiminwa.

“Ni kweli, dawa zinazotumiwa kudhibiti nzige zinaweza kuathiri binadamu na wanyama zikitumiwa vibaya lakini hazisababishi kansa. Watu wana kila sababu ya kuingiwa hofu na kujitahadhari, lakini athari za dawa zinazotumiwa zinaweza kudhibitiwa kwa hivyo jamii isiwe na hofu,” FAO iliambia ‘Taifa Leo’ kupitia kwa taarifa.

Shirika hilo hupendekeza mataifa yaepushe uvamizi ndiposa huwa inatoa ilani mapema kabla nzige wavamie mahali.

FAO ilitoa tahadhari kwamba nzige watakuwepo kwa miezi sita na wasipodhibitiwa, wataongezeka mara 500 kwa idadi.

Kwa mujibu wa shirika hilo la UN, wingu moja la nzige huwa na mamia ya mamilioni ya wadudu hao waharibifu ambao huweza kusafiri kilomita 150 kwa siku. Umbali huo ni kama kutoka Nairobi hadi Narok mjini.

Kwa mujibu wa shirika la kuangazia wanyama la National Geographic, nzige waliweka historia mnamo 1954 wakati wingu moja liliposafiri kutoka kaskazini mashariki mwa Afrika hadi Uingereza.