Makala

NJAA: Mito na maziwa yakauka Baringo na Nakuru miti ikinyauka

March 19th, 2019 2 min read

RICHARD MAOSI NA KEVIN KEMBOI

MAELFU ya watu wanahofia maisha yao baada ya chemchemi za maji na mito kukauka katika Kaunti ya Nakuru na Baringo kutokana na ukame. 

Baadhi ya vyanzo vya mito ni kutoka kwenye msitu wa Mau, mojawapo kikiwa chanza cha Mto Perkerra unaoshuhudia kiwango kidogo mno cha maji msimu huu kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Mto Perkerra umekuwa ukitegemewa na wakulima lakini ishara za hivi punde zinaonyesha hali tofauti wakulima wakikosa maji ya kilimo chao.

Mradi wa kunyunyizia mimea wa Perkerra uliobuniwa mnamo 1954 na serikali ya kitaifa kwa lengo la kuwanufaisha wakazi wa Nakuru na Baringo kupata chakula, sasa hauna msaada kwa wakazi.

Kulingana na meneja mkuu wa mradi huo Enos Wafula, ukubwa wake ni hekta 5000 zinazowafaidi wakulima katika upanzi wa mchele, mahindi, nyanya, vitunguu, matikiti maji na mipapai, lakini mimea hii huenda ikanyauka ikiwa mvua itazidi kuchelewa.

Mkurugenzi mkuu wa Mradi wa Perkerra Enos Wafula akielezea masaibu yanayokumba mradi wa unyunzizaji kwenye Mto Perkerra. Picha/ Richard Maosi

Changamoto ya maji imekuwa ikiwakumba wakulima kuanzia mwishoni mwa 2018. Taifa Leo Dijitali iligundua wakulima wengi wanaotegemea sehemu ya hekta 1500 kunyunyizia mimea yao maji walikuwa na wakati mgumu kukabiliana na makali ya kiangazi.

Mkulima Julius Bartonjo alisema upungufu wa kiwango cha maji unatia shaka ikizingatiwa kuwa wakulima wengi hulisha familia kupitia Perkerra.

Pia Perkerra hutumika kulisha kaunti nzima ya Baringo kwa uzalishaji wa mboga za kawaida na zile za kienyeji.

“Nimekuwa nikitumia kila juhudi kunyunyizia vitunguu vyangu maji, na ninahofia kuwa msimu huu nitapata hasara kubwa kwa sababu ninategemea mto Perkerra, wala sina njia nyingine,” Bartonjo alisema.

Visima vya maji pia vimekauka. Picha/ Richard Maosi

Wakazi wengi wananyoshea kidole cha lawama wale wanaoharibu Msitu wa Mau kwa kuchangia masaibu yanayowakumba.

“Wengi wetu wanategemea maji ya mto Perkerra kufanyia kila kitu. Uharibifu wa mali asilia kama misitu unatuponza,” Bi Caroline Cherono aliongezea.

Aliongezea kuwa serikali inahitaji kuweka mipango kabambe kukabiliana na wale wanaochoma makaa na kuteketeza misitu.

Mto unaopeleka maji katika ziwa la Baringo pia unasambaza maji kwenye miradi mingine ya unyunyizaji kama vile Sandai, Endau, Lororo na Mukutani, eneo kame linalopatikana katika kaunti ndogo ya Marigat.

Sehemu ya mto Perkerra inayotumika kunyunyizia maji kwenye mashamba ya kukuza mimea. Picha/ Richard Maosi

Mara nyingi mto huu huwa umefurika maji, lakini kutokana na kiangazi na uharibifu wa msitu wa Mau,  kiwango cha maji kimepungua sana.

Ndio sababu shughuli za upanzi wa mimea, sasa  zimeanza kutekelezwa kwa zamu ili kutosheleza mahitaji ya maji haba yanayopatikana.

Wafugaji wa kuhamahama nao pia wanategemea maji ya mto wenyewe kunywesha mifugo wao.

Mwenyekiti wa Perkerra aliongezea kuwa upungufu wa maji ulikuwa umeanza kusababisha migogoro baina ya jamii zinazoishi Marigat.

Jamii husika zimekuwa zikiwekeana kisasi dhidi ya kutumia bidhaa hii adimu na wakati mwingi kupigana.

Jua kali linawapa mifugo kiu ya mwaka. Picha/ Richard Maosi

Na si Marigat tu, maeneo jirani ya Molo na Njoro pia yanatatizika kutokana na kiwango cha maji kushuka katika mito yao huku miti ikinyauka vichakani.

Mto Njoro humimina maji ndani ya Ziwa Nakuru, kitovu cha uhai ndani ya mbuga ya wanyama ya Nakuru, na sasa baadhi ya wanyama tayari wameanza kuhama wakisaka makazi yenye maji.

Mito midogo inayoteremsha maji hadi Ziwa Nakuru, pia limekauka na kuwanyima wanyamapori burudani ya kukata kiu.

Kwingineko Mto Weseges unaowapa maji wakazi wa kaunti nne zinazozunguka Nakuru pia umeanza kukauka na kupunguza maji ndani ya Ziwa Baringo.

Sehemu ya mto Perkerra inayoashiria kupungua kwa kiwango cha maji eneo la Marigat. Picha/ Richard Maosi

Maziwa mengine makuu yanayoshuhudia kiwango cha maji kushuka ni Bogoria, Naivasha na Baringo.

Taifa Leo Dijitali pia ilibaini eneo la Rongai, kaunti ndogo ya Nakuru lilikuwa limepata pigo baada ya kugeuka jangwa bila kutarajia .

Wakulima wengi hapa wamekuwa wakiunganisha maji moja kwa moja kutoka mtoni, licha ya marufuku kutoka kwa serikali.

Kiwango cha maji kwenye visima mjini Nakuru na Baringo vilevile vinaashiria hali ya kunyauka.

Awali mto huu ulikuwa umefurika maji. Picha/ Richard Maosi

Wastawishaji wa kibinafsi sasa wanatafuta njia mbadala ya kukidhi mahitaji ya viwanda huku wakazi wa mitaa ya Kampi ya Moto, Kiamunyi na Rongai nao waking’ang’ania maji ya wachuuzi.