Njaa na Ukame: Baadhi ya wakazi wa Magarini walazimika kula mizizi hali ikizidi kuwa mbaya

Njaa na Ukame: Baadhi ya wakazi wa Magarini walazimika kula mizizi hali ikizidi kuwa mbaya

NA ALEX KALAMA

WAKAZI wa Magarini kaunti ya Kilifi sasa wanaitaka serikali kusambaza chakula cha msaada kwa dharura ili kuwanusuru dhidi ya makali ya njaa na ukame.

Wakiongozwa na Bw Elias Kitsao, wamesema hali ya kiangazi kikali inayoshuhudiwa kwenye maeneo ya Changoto, Kadzandani, Kamale, Mtoroni, Dhololo Bula, Mulunguni, Mwele na Mtoroni imesababisha wakazi wengi kuhangaika wakitafuta chakula baada ya mvua kukosekana kwa muda mrefu katika maeneo hayo.

“Kweli njaa imekithiri hapa Magarini kusema kweli tunapata shida kwa sababu mvua haikunyesha na hakuna chakula. Watoto nao wameanza kukonda. Naomba serikali ituonee huruma itusaidie maana tunaumia,” alisema Bw Kitsao.

Wakazi hao sasa wanasema kwamba wanalazimika kula mizizi ya misituni ili kupunguza makali ya njaa huku watoto wao wakiathirika kiafya kutokana na ukosefu wa chakula.

“Kusema kweli kiangazi kimezidi na hata mifugo inakufa. Watu wa kule Adu wanakula mizizi. Tafadhali tunaomba serikali mpya ambayo imeingia ituangalie watu wa Magarini tunaumia,” alisema Bw Kitsao.

Kwa upande wake chifu wa eneo la Adu Shedrack Maneno amesema hali hiyo imechangiwa na kipindi kirefu cha ukame.

Afisa huyo wa utawala ameliomba Shirika la Chakula Duniani (FAO) kwa ushirikiano na wadau wengine kujitolea kuwasaidia wananchi wanaopitia hali ngumu ya maisha kwa kuwapa chakula cha msaada.

“Ukiangalia hali ilivyo kwa sasa ni watu wengi sana,ambao wako katika hali ya kutaka kusaidiwa ili waweze kupata chakula. Tunaomba wahisani waweze kujitokeza na kusaidia maana naona ikiwa hatua za haraka hazitaweza kuchukuliwa kuikabili hii hali, basi huenda wengine wakafa na njaa,” alisema Bw Maneno.

Hata hivyo Maneno ameitaka serikali ya kaunti hiyo kupitia idara ya kukabiliana na majanga kufanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba imesambaza chakula kwa wale wote walioathirika na ukame eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Idadi ndogo ya wenyeji chuoni yamkera gavana

Omanyala, Okutoyi washauri wanatenisi chipukizi jinsi ya...

T L