Njaa: Serikali kuanza kusambaza mlo, maji

Njaa: Serikali kuanza kusambaza mlo, maji

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI kuu itaanza kuwapa msaada wa chakula na maji wanaoathiriwa na njaa kuanzia wiki ijayo, ili kuokoa maisha baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutaja baa la njaa kuwa janga.

Kulingana na Naibu Waziri wa Ugatuzi na Maeneo Kame, Bw Gideon Mung’aro, serikali itawasaidia waathiriwa wote wa baa la njaa.

Akiwajibu viongozi wa Pwani kwenye mkutano wa kisiasa katika ukumbi wa Wild Waters huko Mombasa waliolalamika kuhusu baa la njaa linaloendelea kuathiri sehemu hiyo, Bw Mungaro alisema waathiriwa pia wanaendelea kupewa pesa.

“Tunataka kuwahakikishia ya kwamba tuko na mikakati kabambe kuna wale wanatumiwa pesa kwa njia ya simu lakini kama vile Rais Kenyatta alivyotangaza juzi kuhusu mambo ya njaa, kuanzia wiki ijayo mtaona tukianza kupeana vyakula vya msaada na maji kwa walioathirika ili wasife njaa,” alisema Bw Mung’aro.

Alisema baadhi ya mawaziri akiwemo Bw Eugene Wamalwa, manaibu wao na maafisa wengine serikalini wataanza kuzunguka sehemu mbali mbali nchini kuhakikisha Wakenya wanapewa vyakula na maji ili wasife njaa.

“Mbali na kupeana vyakula na maji serikali inaweka mikakati zaidi kuhimili sehemu kame. NDMA itaanza kupeana vyakula na maji sehemu za Kilifi, Kwale, Tana River,” alisema.

Hata hivyo, Bw Mung’aro aliwataka viongozi wa pwani kuweka mikakati ya kuhakikisha uwepo wa chakula kukabiliana na swala la ukame.

Alisema Wizara ya Kilimo imegatuliwa hivyo basi viongozi hao wanafaa kujizatiti kuweka suluhu la ukame.

“Magavana wa kaunti za Pwani tuweke usalama wa chakula kwa watu wetu. Ajenda yetu haitakuwa kugawanya chakula kwa watu wetu kila mara, tuangalie kaunti zetu za pwani zinaweka mikakati gani kuhakikisha watu wetu wanazalisha vyakula,” alisema.

Haya yanajiri baada ya viongozi wa Pwani kulalamika kuhusu baa la njaa linaloendelea kuwaathiri wakazi wa ukanda huo.

“Rais Uhuru Kenyatta alitaja baa la njaa kama janga la dharura (national disaster); tunataka waathiriwa wapewe chakula na maji,” alisema mbunge wa Garsen Bw Ali Wario.

Mwenzake wa Ganze Teddy Mwambire aliisihi serikali kuu kuweka mikakati ya kudumu kukabiliana na janga hilo ambalo limeathiri wakazi wengi

“Swala la baa la njaa limekithiri, ni wakati mwafaka kwa serikali kuweka mikakati ya kudumu kukabiliana na swala hili. Wahanga wapewe chakula na maji lakini tunataka suluhu,” alisema.

Kulingana na Halmashauri ya Kitaifa ya Kukabiliana na (NDMA) zaidi ya watu laki 400,000 eneo la Pwani wanahitaji chakula.Kilifi, Kwale, Tana River na Lamu zilitajwa kuwa miongoni mwa kaunti 23 hatari nchini zinazokabiliwa na baa la njaa.

Kulingana na NDMA takriban watu 2.1 milioni wanakabiliwa na baa la njaawakihitaji vyakula vya dharura.Kaunti zengine zinazokodolea macho njaa ni pamoja na Baringo, Kajiado, Kwale, Laikipia, Lamu, Makueni, Meru, Taita Taveta, Tharaka Nithi na Pokot Magharibi.

You can share this post!

PSG yapepeta Lyon kwenye mechi ya kwanza ya Messi katika...

Wanasiasa wang’ang’ania mahasla