Njaa: UN yaahidi Sh13b kusaidia waathiriwa

Njaa: UN yaahidi Sh13b kusaidia waathiriwa

GEORGE MUNENE na BARNABAS BII

UMOJA wa Mataifa (UN) umeahidi kutoa Sh13 bilioni kusaidia watu milioni 2 wanaokabiliwa na janga la njaa nchini.

Msemaji wa Serikali Kanali Cyrus Oguna, Jumapili alisema kwamba Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limetoa Sh350 milioni ili kununua lishe ya mifugo katika maeneo yanayokumbwa na ukame.

Bw Oguna alisema serikali imetenga Sh2.4 bilioni kununua vyakula ili kuwalisha Wakenya waliokumbwa na baa la njaa.

Akizungumza wakati wa mchango wa Harambee katika kanisa la Anglikana la Good Samaritan Difathas, Kaunti ya Kirinyaga, Bw Oguna alisema tayari serikali imetumia fedha kuwanunulia baadhi ya Wakenya vyakula huku akikiri kuwa ukame huo unatisha na lazima mikakati faafu iwekwe kuyaokoa maisha ya watu.

Kanali Oguna alisema ni kaunti 20 ambazo zinakabiliwa na njaa huku nusu ya idadi hiyo ikiwa zile ambazo zimeathirika sana na zinahitaji msaada wa kidharura.

Msemaji huyo alikariri kuwa serikali inamakinika kuhakikisha kuwa wale ambao wanakabiliwa na njaa hawapotezi maisha yao na wanafikiwa na misaada ya vyakula, maji na mahitaji mengine ya kimsingi.

“Kumekuwa na misimu miwili ambapo mvua haijanyesha ndio maana kuna ukame. Wakenya wengi hawakuvuna chochote na sasa hawawezi kujilisha huku mifugo pia wakiathirika,” akasema.

Tayari baadhi ya mifugo ikiwemo ngamia, ng’ombe na mbuzi wamekufa baada ya kulemewa na makali ya njaa huku wafugaji wakiitisha msaada kutoka kwa serikali kununua mifugo yao.

Kanali Oguna alikuwa ameandamana na Gavana wa Laikipia Nderitu Muriithi pamoja na aliyekuwa msaidizi wa kibinafsi wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, Bw Ngari Gituku.

Pia alitaka Wakenya wadumishe amani na kuwaonya wanasiasa dhidi ya kueneza chuki kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Kauli ya Kanali Oguna kuhusu njaa inajiri wakati ambapo janga la kitaifa linanukia Kaskazini mwa Kenya ambapo maelfu ya familia wanakodolewa macho na mauti kutokana na ukosefu wa chakula, watoto pia wakiathirika na utapiamlo.

Ripoti iliyotolewa na Wizara ya Afya kupita kamati inayoshughulikia utoshelevu wa chakula nchini, ilionya kuwa kuna hatari ya kutokea kwa janga la kitaifa iwapo familia kwenye kaunti za Samburu, Marsabit, Isiolo, Garissa, Mandera na Wajir hazitafikiwa na kupewa vyakula.

Hasa ripoti hiyo inasisitiza kuwa watoto 8,000 na akina mama 5,365 katika Kaunti ya Turkana wanakabiliwa na utapiamlo huku hatua za dharura zikihitajika kuwapa vyakula venye madini ya vitamin A, dawa ya minyoo na maziwa kwa watoto wadogo.

Mbunge wa Turkana Kaskazini Christopher Nakuleau naye ameiomba serikali iharakishe kugawa vyakula kwenye maeneo hayo ili kuzuia vifo ambavyo vinanukia.

“Hali huenda ikawa baya zaidi iwapo ukame utaendelea kushuhudiwa. Wakazi wanategemea sana maziwa na nyama kutoka kwa mifugo yao ambao sasa pia wamedhofika kutokana na ukosefu wa lishe,” akasema Bw Nakuleau.

Serikali nayo imetenga Sh1.5 bilioni kugharimia vyakula kwa familia zinazokabiliwa na njaa.

Kinaya ni kwamba wakulima wa mahindi Kaskazini mwa Bonde la Ufa nao wanalalamika kuwa wana mahindi mengi ila hakuna soko kutokana na uagizaji wa mazao hayo mengi kutoka nje ya nchi.

You can share this post!

Kaparo atawazwa msemaji wa jamii yake Laikipia

‘Sherehe’ kwa walevi baa 1,800 zikitakiwa kuuza...