Habari

Njaa yabisha nzige wakitua Kirinyaga

January 13th, 2020 1 min read

Na GEORGE MUNENE

HOFU ya njaa imezuka katika eneo la kati baada ya nzige kuonekana katika kijiji cha Riandira, Kaunti ya Kirinyaga Jumatatu.

Wakazi wana wasiwasi kwamba wadudu hao waharibifu huenda wakaenea eneo zima la Kati na kuharibu mazao ya mahindi, mpunga, majani chai na kahawa.

Nzige tayari wamevamia mashamba ya wakulima wawili eneo la Riandira.

“Wamo katika shamba langu. Wanakula majani katika miti yangu na wanaenea kwa kasi,” mmoja wa wakulima, Bw Isaack Ndung’u akasema.

Bw Ndung’u alisema nzige hao walifika Jumapili jioni na wakaanza kuingia katika shamba la mahindi.

Mkulima mwingine, Bw Sospeter Kariuki alieleza jinsi nzige walivyowasili wakiwa wengi na kusababisha hofu kwa wakazi.

“Kila mtu anaogopa na serikali inafaa ichukue hatua za haraka kudhibiti hali hii kabla janga litokee,” akaongeza Bw Kariuki.

Kiongozi wa wengi katika bunge la Kaunti ya Kirinyaga, Bw Kamau Murango alitoa wito hatua zichukuliwe kwa dharura.

“Nimepokea habari pia kwamba nzige walionekana sehemu mbalimbali za eneo hili. Kama hatua za dharura hazitachukuliwa, hili litakuwa janga,” akasema.

Bw Murango aliongeza kwamba nzige walionekana katika Kaunti za Isiolo, Meru, Laikipia na Marsabit na sasa wanaenea Kirinyaga.

“Tuna wasiwasi pia sisi kama viongozi kuhusu uvamizi huu wa nzige katika eneo hili. Wakazi wanategemea kilimo kimaisha na kama mazao yao yataharibiwa, watateseka,” akasema Bw Murango.

Nzige hao waliingia Kenya mwezi uliopita wakitokea Ethiopia na kwanza walivamia kaunti za Mandera na Wajir.

Nzige hao huharibu kila aina ya mimea maeneo wanayovamia.