Njaa yalemea raia msaada wa serikali ukichelewa kufika

Njaa yalemea raia msaada wa serikali ukichelewa kufika

WANANCHI katika maeneo mbalimbali nchini wanazidi kutaabika kwa kukosa chakula na maji, huku maswali mengi yakiibuka kuhusu matumizi ya pesa ambazo hutengwa kila mara kutafuta suluhu ya janga la kiangazi na ukame.

Kwa jamii za wafugaji, ukosefu wa mvua ya kutosha kwa mwaka wa nne sasa umesabisha hasara ya mamilioni ya pesa kutokana na vifo vya mifugo.

Bw Amos Kitili, 65, kutoka Kaunti-ndogo ya Mashuru, Kajiado, anasema ashapoteza takriban ng’ombe 50 kwa miezi mitatu iliyopita.

Mizoga ya mifugo imetapakaa katika eneo hilo, sawa na hali ilivyo katika maeneo mengine kame katika kaunti za kaskazini, mashariki na Pwani ya Kenya.

“Ng’ombe hao waliofariki wangeniletea zaidi ya Sh2 milioni kama ningewauza sokoni. Watoto wangu washafukuzwa shuleni kwa kukosa karo,” akasema.

Mbali na mifugo, wanyamapori pia wanazidi kuangamia huku ndovu wakivamia vijiji kutafuta lishe na maji.

“Hili ni janga kubwa ambalo hatujashuhudia kwa zaidi ya miaka 10. Serikali lazima itafute mipango ya kusaidia wafugaji kurudisha mifugo wao baada ya ukame,” akasema Bi Emily Mayian ambaye ni mkulima.

Watoto katika maeneo mengi yaliyoathirika wameacha kwenda shuleni kwa sababu ya njaa. Wengine wameona heri waende kusaidia kutafuta chakula na maji kuliko elimu.

Wadau wengine pia wameeleza hofu ya uwezekano wa vurugu za kijamii waking’ang’ania rasilimali chache zilizopo.

MGAO KWA AJILI YA KUKABILI JANGA

Katika Kaunti ya Tana River, madiwani wameitaka serikali ya kaunti hiyo kueleza kwa kina jinsi Sh132 milioni za kukabiliana na janga la ukame zilivyotumika.

Madiwani hao wanahofia kuwa huenda pesa hizo zilizotengwa kipindi cha fedha cha mwaka wa 2021/2022 zilifujwa kwani hakuna ithibati zozote mashinani kuhusu matumizi yake.

Vilevile, wanasema serikali ya kaunti hiyo haijatoa ripoti ya maelezo ya matumizi ya fedha hizo kwa bunge la kaunti hadi sasa.

Wakiongozwa na diwani wa wadi ya Hirimani, Bw Ishamael Kodobo, viongozi hao wamedai kuwa afisi ya gavana imewachezea shere, huku ukame ukiendelea ‘kugaragaza’ kaunti hiyo.

“Hii ni mipango ya serikali na lazima pawepo thibitisho la matumizi ya pesa hizo. Katika msimu uliopita, nilitumia pesa zangu kuwatafutia watu wangu maji. Chakula cha msaada walipewa na mashirika ya kibinadamu, sikuona mkono wa Kaunti pale,” akasema Bw Kodobo.

Aliendelea kuwa iwapo pesa hizo zingetumika kwa njia sawa, basi wananchi hawangekuwa wakilalamika kuhusu njaa hivi sasa.

Kulingana naye, misaada ilitoka kwa mashirika kama Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Ukame (NDMA), lakini sio Kaunti.

Zaidi, viongozi hao wanadai kuwa mhasibu wa idara ya mipango ya dharura, mpaka sasa hajaitikia wito wa bunge hilo ili kuweka wazi maswala kuhusiana na pesa hizo.

“Tusemezane ukweli, hata wakulima shambani hawakuuza mazao yao kwa kaunti. Chakula kilichokuwa kwenye maghala twafahamu sote kuwa kililiwa wakati wa uchaguzi,” alisema Bw Ali Juma, wa wadi ya Madogo.

Awali Gavana Dhadho Godhana alidai kuwa pesa zilizotengwa kwa ajili ya janga hilo ziliisha kabla ya uchaguzi.

Mhasibu wa Idara ya Mipango ya Dharura katika kaunti, Bi Salma Makuru hata hivyo amekana ubadhirifu wa pesa hizo.

“Waliniita pale mwanzo kabla ya uchaguzi, na nikawaelezea changamoto zilizokuwepo na matakwa ya Mhasibu Mkuu wa Serikali kuhusu sheria ya matumizi ya pesa hizo,” alieleza.

Bi Makuru hata hivyo amewahakikishia viongozi hao kuwa wakaazi watapata msaada kwa wakati ufaao pindi tu, bajeti itakapopitishwa na kuwasilisbwa kwa mhasibu mkuu wa serikali.

  • Tags

You can share this post!

Wawili ndani miaka 30 kwa kuiba teksi kimabavu

Wachukuzi walia SGR ikiwanyima biashara

T L