Dondoo

Njaa yasukuma pasta ukutani

May 26th, 2020 1 min read

Na CORNELIUS MUTISYA

MISUUNI, MACHAKOS

PASTA wa kanisa moja eneo hili aliamua kuuza vyombo vya muziki ili ajikimu kimaisha baada ya Covid-19 kumlemaza kiuchumi.

Kulingana na mdaku wetu, pasta alifungua kanisa miaka minne iliyopita na akajishindia wafuasi chungu nzima.

Inaarifiwa kwamba, waumini waliandaa harambee ya kuchanga pesa za kupanua kanisa ili liweze kuwatoshea na wakatenga kiasi fulani kununua vyombo vya muziki na kuhubiri.

”Waumini walijenga kanisa la kisasa na wakanunua vyombo vipya vya kuporomosha muziki,” asema mpambe wetu.

Hata hivyo, janga la corona liliporipotiwa nchini na serikali ikatangaza sheria kali za kulitokomeza, ikiwemo kufunga makanisa, maisha ya pasta huyo yalidorora sana.

”Kufungwa kwa makanisa kutokana na corona kulimwathiri mno mtumishi wa Mungu. Waumini walikoma kabisa kutoa sadaka, fungu la kumi na matoleo mengine ya kusukuma huduma,” asema mdokezi.

Pasta alikosa pesa za kukidhi mahitaji ya familia yake na hakuweza kuwaendea waumini ambao pia wamelemewa na gharama ya maisha.

Inasemekana pasta aliamua liwe liwalo na akauza vyombo vya muziki ili apate hela za kukidhi mahitaji ya kimsingi maishani. Aliona ni heri lawama kuliko fedheha! Kulingana na mdokezi, waumini waliposikia habari hizo walifadhaika mno na wakatisha kutorejea kanisani humo baada ya janga la corona kudhibitiwa.

”Kwa sasa hatuna hatua ya kumchukulia pasta wetu maana ibada zimesitishwa kote nchini. Hata hivyo, huenda sote tukahama kanisa hilo makanisa yakifunguliwa,” akasema mshiriki mmoja wa kanisa hilo.