Habari Mseto

Njama mpya ya matapeli kutumia picha za wagonjwa kupora wahisani

April 23rd, 2019 1 min read

NA AGEWA MAGUT

WALAGHAI wanaendelea kutumia mitandao ya kijamii nchini kuchapisha visa vya uongo ili kupata fedha kutoka kwa Wakenya wakarimu wanaosikitikia visa hivyo vinavyosawiriwa kama vinavyohitaji misaada ya kidharura.

Hii ni baada ya wahuni hawa kugundua kuwa Wakenya wamekuwa na ada ya kutoa pesa kwenye kampeni za misaada zinazoandaliwa kama mashindano ya mbio ya Beyond Zero, Mater Heart Run na Kenyans for Kenyans ambazo huchangisha mamilioni ya fedha.

Ulaghai huo sasa umechukua mwelekeo mpya baada ya kuibuka kwa kundi moja la wasanii linaiba picha za wagonjwa wanaogua hospitalini, kuziweka mitandaoni kisha wanaandika habari za kusikitisha za kuwapa watu msukumo wa kutoa fedha.

Uchunguzi wa TaifaLeo ulifichua jinsi mtumiaji wa Facebook kwa jina Dinnah Kadasira ambaye tayari amefuta akaunti yake, amekuwa akiitisha misaada ili ‘kulipa’ gharama ya matababu kwa mgonjwa kwa jina Lavenda ambaye anadai anaugua saratani katika hospitali ya Kenyatta.

Kando na picha hiyo, yeye huweka picha za wagonjwa wengine katika mitandao mbalimbali za kijamii japo kinaya ni kwamba nambari ya kutuma fedha kupitia mtindo wa Mpesa na ile ya Paybill ni sawa katika picha hizo zote.

Uchunguzi wa TaifaLeo pia ulibaini kwamba Bi Kadasira ana akaunti nyingine iliyosajiliwa kwa jina la Dibo Sankala Sama.

Taifa Leo ilipopigia simu ikitumia nambari zilizowekwa ili kubaini ukweli, mwanaume ndiye alipokea kwa kusitasita na kusema “Linda hayuko, ametoka kidogo.”