Njama mpya yachorwa kutimua Ruto Mlima Kenya

Njama mpya yachorwa kutimua Ruto Mlima Kenya

Na MWANGI MUIRURI

WANASIASA wa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta eneo la Mlima Kenya wamezindua njama mpya ya kumkata mbawa Naibu Rais William Ruto.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth na aliyekuwa Mbunge wa Maragwa, Elias Mbau, mpango huo unahusu kubuniwa kwa jopo la wanasiasa kutoka kila kaunti.

Njama hiyo inalenga kupunguza umaarufu ambao Dkt Ruto amekuwa akifurahia eneo hilo.

Duru zilieleza kuwa hii ni mojawapo ya njama ya rais ya kumtenga naibu kote nchini kwa kuwatumia wanasiasa walio na ushawishi katika makabila yao.

Mrengo wa One Kenya Alliance unaoshirikisha Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula na Gideon Moi unatarajiwa kumzima Dkt Ruto katika maeneo ya Ukambani, Magharibi na baadhi ya sehemu za Rift Valley.

Kwa upande mwingine, Kiongozi wa ODM Raila Odinga anachezeshwa kulinda ngome yake ya Nyanza ili Dkt Ruto asipenye huku Gavana Hassan Joho wa Mombasa akitarajiwa kuongoza wenzake Salim Mvurya, Amason Kingi na Granton Samboja kumfungia nje Dkt Ruto eneo la Pwani.

Katika kuondoa ushawishi wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya, wanamikakati wa Rais Kenyatta wanapanga kubuni jopo la wanasiasa, hasa magavana, wakiwa na majukumu kushawishi wakazi wa maeneo yao kutomuunga mkono naibu rais.

Bw Mbau aliambia Taifa Leo kuwa wanaopendekezwa kuwa katika jopo hilo ni magavana Nderitu Muriithi wa Laikipia, Anne Waiguru (Kirinyaga), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi), Kiraitu Murungi (Meru) na Lee Kinyanjui wa Nakuru.

Wengine ni Rais Kenyatta akiwakilisha Kiambu, Kenneth (Murang’a), aliyekuwa Mbunge wa Dagoretti Kusini, Dennis (Nairobi), Spika Justin Muturi (Embu), Mbunge wa Kipiri Amos Kimunya (Nyandarua) na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe awakilishe Nyeri.

Bw Kenneth alisema lengo la mpango huo ni kuunganisha jamii za Mlima Kenya ziwe na usemi mmoja katika uchaguzi wa 2022.

Lakini wafuasi wa Dkt Ruto wakiongozwa na Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua, wamepuzilia njama hiyo wakisema itafeli kwa kuwa haishirikishi wananchi mashinani.

You can share this post!

HAKUNA PUMZI

Jaji Mkuu: Uamuzi wa usiku watatiza Koome