Siasa

Njama ya kusambaratisha Mlima Kenya haitoboi – Gachagua

June 2nd, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Bw Rigathi Gachagua ameteta kwamba kuna njama inayosukwa na baadhi ya wasaliti wa kisiasa walio na asili ya Mlima Kenya kwa ufadhili wa wengine kutoka nje ya eneo hilo kutawanya kura za wenyeji.

Akiongea na wenyeji wa mji wa Limuru mnamo Mei 31, 2024, katika mkutano wa hadhara, Bw Gachagua alilia kwamba yeye kama kinara wa siasa za Mlima Kenya atapambana kufa kupona kuhakikisha kwamba njama hiyo haifaulu.

Alisema kwamba njama iliyoko ni ya kuondoa jamii za Mlima Kenya kutoka ndani ya serikali, akiapa kutokubali hilo litimie.

“Kuna baadhi yetu ambao ni wasaliti wa kijamii na ambao wakipewa kopo la kileo hukubali kutumwa hapa kuja kusambaza utengano. Wanalala wakiwa na sikio lao nyanjani wakitusikiliza ndipo watusaliti. Mkiwaona na muwatambue, waambieni kwamba mimi kama kiongozi wenu mkuu eneo hili nimeagiza wakemewe,” akasema Bw Gachagua.

Alisema kwamba ni kwa msingi wa kuunganisha wenyeji wa Mlima Kenya ambapo huwa anaomba msamaha wa kijamii kwa familia ya mwanzilishi wa taifa la Kenya Mzee Jomo Kenyatta “kwa maovu ya kimaongezi ambayo tuliielekeza wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2022”.

“Hatutawahi tena kutengana kiasi kwamba tunararuana na kupapurana kama majibwa… Tutaungana sote ndio nikifanikiwa kuchota kwa serikali kuu, niwe nikiwaletea hapa mashinani. Tunaelekezewa vita hivi ndio nikose uwezo wa kudai haki yenu ya mgao wa keki ya kitaifa. Umoja wetu ndio tu ngao yetu katika misukosuko ya kisiasa,” akasema.

Alisema kwamba kosa si kosa bali kosa ni kulirudia kosa hilo ikiwa na maana kwamba “hatutawahi kama jamii kujipata katika soko la kukemeana na kurushiana cheche za matusi jinsi tulivyofanyia familia hiyo ya Kenyatta ambayo ni ya dada yangu Mama Ngina Kenyatta”.

Bw Gachagua alisema kwamba eneo la Mlima Kenya huwa na maadui wengi ambao wanajua kwamba mbinu tu ya kukabiliana na uthabiti wao ni kupitia kuwatenganisha kimaeneo.

“Tuko na vijana hapa ambao wanaanza hadithi za mabadiliko wakiuza sera za migawanyiko hata ya kizazi. Kunao wanasema watu wa Kiambu washawahi kuwa na uongozi kwa hivyo wajiondoe kwa siasa za 2027 na 2032…wengine wanasema Nyeri ishawahi kuwa na viongozi kwa hivyo ifuate mkondo wa kujitenga…hayo ni mawazo duni ambayo hayatusaidia,” akasema.

Bw Gachagua alikariri hatari za migawanyiko kuwa na ushahidi ndani ya chaguzi za 1992 na 1997 ambapo licha ya wenyeji Mlima Kenya kuwa na wingi wa kura, Rais wa wakati huo Daniel Moi aliendelea kutawala kwa kuwa wawaniaji wa asili ya Mlima wakiwa ni Kenneth Matiba na Mwai Kibaki waligawanyika.

“Ikiwa tutatengana, huu ufalme wenu nilio nao kwa sasa tutakuwa tukiuonea kwa mitandao ya kijamii ukiwa mikononi mwa wengine. Hali ilivyo kwa sasa ni ile ya kujaribu juu chini kututenganisha ndio turudi kwa ule ujinga wetu wa 1992 na 1997,” akasema.

Ili kujithibiti katika safu ya kisiasa, alisema kwamba jamii za Mlima Kenya zinahitaji kuwa na wingi.

“Ndio sababu mimi nawasihi mzaane kwa wingi. Zaaneni kwa kuwa watoto ni wazuri na ndio kesho yetu. Tunahitaji wingi ndio tuwe na uwezo wa kuingia kwa soko la siasa kudai asilimia ya wingi wetu katika manufaa,” akasema.