Njama ya serikali kuandaa refarenda yafichuka

Njama ya serikali kuandaa refarenda yafichuka

Na WANDERI KAMAU

IMEBAINIKA serikali inaendesha njia za kichinichini kuandaa kura ya maamuzi kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Hii inaonekana kama njia ya kuhakikisha ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) imepita, licha ya vikwazo vinavyoonekana kuiandama.Kwenye bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Ukur Yatani, Alhamisi, serikali iliitengea Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Sh15 bilioni.

Kiwango hicho ni mara tatu zaidi ya fedha ambazo tume hiyo ilitengewa kwenye mwaka wa kifedha wa 2020/2021.Mwaka uliopita, tume ilitengewa Sh4.6 bilioni.Tume hiyo pia imetengewa Sh100 milioni kuendesha shughuli za ugavi wa mipaka.

Mnamo Aprili, tume pia ilitangaza kandarasi ya kununua mitambo mipya ya kuandaa uchaguzi.Hata hivyo, Bw Yatani hakutaja ikiwa fedha hizo ni za kuiwezesha tume kuandaa kura hiyo.Hatua hiyo inajiri huku mawakili wanaowawakilisha Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga wakiwasilisha rufaa zao katika Mahakama ya Rufaa, kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kuharamisha mchakato huo.

Licha ya uamuzi huo, viongozi hao wamekuwa wakionekana kufanya kila wawezalo kuhakikisha mchakato umefaulu.Baadhi ya juhudi za Rais Kenyatta zinazoonekana kama njia ya kushinikiza kura hiyo ni kuharakisha kuapishwa kwa majaji 34 kati ya 40 walioidhinishwa kuteuliwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) mnamo 2019.

Wiki iliyopita, Bw Odinga aliwahakikishia wafuasi wake kwamba “mchakato huo bado unaendelea.”“Raggae haijasimama. Itarejea hivi karibuni,” akasema Bw Odinga alipohutubu katika Kaunti ya Kisumu.

Kwenye hotuba yake wakati wa sherehe za Sikukuu ya Madaraka jijini Kisumu, Rais Kenyatta aliishambulia vikali Idara ya Mahakama, akisema haifai kuwa kikwazo “kuwawezesha Wakenya kuelekea wanakotaka.”

Wadadisi wanasema wawili hao wako tayari kufanya wawezalo kuona mpango huo umefaulu, ikizingatiwa ni kama mradi wao binafsi.“BBI ni mchakato ulioanzishwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga. Hivyo, hawako tayari kuona ukisambaratishwa na maamuzi ya mahakama,” asema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa.

  • Tags

You can share this post!

Kenya yakopa Sh80b baada kutangaza bajeti ya madeni

Wakili wa Ruto kuapishwa wiki ijayo kumrithi Bensouda