Njama ya UDA kumeza vyama tanzu katika Kenya Kwanza yafichuka

Njama ya UDA kumeza vyama tanzu katika Kenya Kwanza yafichuka

NA MOSES NYAMORI

NJAMA fiche imeanzishwa ya kuvunjwa kwa vyama vyote tanzu katika Kenya Kwanza na kuviunganisha na chama cha United Democratic Alliance (UDA), chake Rais William Ruto.

Kama hatua ya kuvishawishi vyama vingine 13 kufuata mkondo huo, Chama Cha Kazi (CCK) kinachoongozwa na Waziri mteule wa Biashara, tayari kimewasilisha ombi kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa kikitaka kiondolewe katika sajili ya vyama vya kisiasa nchini.

Mpango huu unampa Rais Ruto nafasi nyingine ya kuunda chama kikubwa cha kisiasa, sawa na Jubilee iliyobuniwa Septemba 16, 2017. Hii ni kufuatia hatua ya kuunganishwa kwa vyama 13 vilivyokuwa vishirika katika uliokuwa muungano wa Jubilee, alioutumia yeye na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta kushinda urais 2013.

Hata hivyo, jana Jumamosi vyama vingine shirika katika muungano wa Kenya Kwanza (KKA) vilikana madai ya uwepo wa mipango ya kuvunjwa kwavyo ili viwe sehemu ya UDA.

Baadhi ya maafisa wa vyama hivyo walishikilia kuwa vitaendelea na shughuli kama vyama huru.

Aidha, maafisa hao wa ANC na Ford Kenya, walisema kuwa vyama hivyo vitadhamini wagombeaji katika chaguzi ndogo za useneta katika kaunti za Bungoma na Elgeyo Marakwet na maeneobunge ya Garissa Mjini na Kandara.

Baadhi ya wanachama wa UDA, hata hivyo, walionekana kushinikiza kuvunjiliwa mbali kwa vyama hivyo ili kumwezesha Rais Ruto “kufikia malengo yake ya kujenga chama kikubwa kisicho cha kikabila.”

“Wale wote walioteuliwa mawaziri watavunja vyama vyao ili tuwe na chama kimoja na serikali moja. Kuria tayari ameonyesha mfano wa kufikiwa kwa azma hii,” mbunge mmoja wa UDA akasema.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina alisema chama hicho hakina nia ya kuvilazimisha vyama shiriki kuvunjiliwa.

Alisema uamuzi kama huo ni wa hiari.

Lakini Bi Maina alikuwa mwepesi kusisitiza kuwa “itakuwa vizuri kwa viongozi wa vyama hivyo kujiondolea mzigo wa kuendesha vyama vyao.”

“Chama Cha Kazi ndicho chama cha kipekee ambacho kimejitokeza kuunga mkono wazo la kuungana na UDA. Walileta stakabadhi fulani za kufanikisha mpango huo lakini hatukuwa na wakati wa kuzikagua kwa sababu sote tulikuwa tukielekea Bungeni kwa hotuba ya kwanza ya Rais,” Bi Maina akaambia “Taifa Jumapili” kwa njia ya simu.

“Wamewasilisha notisi kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa wakitaka kujiunga na nasi. Ni uamuzi wa hiari na hatuwezi kuwazuia kujiunga na chama kikubwa. Ni wazo zuri kwa mtu ambayo ameteuliwa Waziri kujiondolea majukumu ya kuendesha chama na kuelenga majukumu mapya ya uwaziri,” Katibu huyo mkuu, ambaye ni Seneta Maalum, akaeleza.

Jana Jumamosi, Bw Kuria ambaye ni mbunge wa zamani wa Gatundu Kusini, alifafanua kuwa uamuzi wa kuvunjwa kwa CCK uliidhinishwa na Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la chama hicho.

“Huu sio uamuzi wa mtu mmoja au wanachama wachache. Ulijadiliwa na kupitishwa katika NEC yetu iliyofanyika Jumanne wiki hii,” akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Ruto alivyokwepa ulaghai wa kisiasa

AS Roma ya kocha Jose Mourinho yazamisha chombo cha Inter...

T L