Njama ya Uhuru kubomoa Ruto yafichuka

Njama ya Uhuru kubomoa Ruto yafichuka

Na BENSON MATHEKA

MIKAKATI ya Rais Uhuru Kenyatta ya kubomoa umaarufu ambao Naibu Wake William Ruto amejenga eneo la Mlima Kenya imeanza kubainika na kuzaa matunda.

Wadadisi wanasema kwamba japo Dkt Ruto alionekana kuteka eneo la Mlima Kenya kupitia kampeni yake ya hasla ambayo amekuwa akiendeleza kwa miaka minne iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta ameanza kukunjua kucha zake katika juhudi za kumzima.

Wawili hao walitofautiana Rais Kenyatta aliposalimiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga na mchakato wa kubadilisha katiba ambao walianzisha.

Washirika wa Rais Kenyatta wamekuwa wakimlaumu Dkt Ruto kwa kumdharau kiongozi wa nchi na kumsawiri kama aliyeshindwa kusaidia ngome yake ya kisiasa tangu handisheki yake na Bw Odinga.

Kupitia kampeni yake, Dkt Ruto alionekana kugawanya eneo la Mlima Kenya huku akimlaumu Rais Kenyatta kwa kutekeleza ajenda za serikali ya Jubilee kwa kuzingatia mageuzi ya katiba ili kumsaidia Bw Odinga kushinda uchaguzi wa urais wa mwaka ujao.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba wakati Dkt Ruto alikuwa akichafua ngome yake ya Mlima Kenya akijisawiri kama anayefaa kumrithi, Rais Kenyatta alikuwa akisuka mikakati ya kuzima umaarufu wake sio tu eneo la Mlima Kenya bali kote nchini.

“Bila kujitokeza hadharani kuzuru eneo la Mlima Kenya, Rais Kenyatta alihakikisha kuwa ametekeleza miradi yake na kuanza kampeni chini ya maji ya kutetea utenda kazi wake. Miradi mingi imekamilika na anatumia inayoendelea kumbomoa Dkt Ruto kwa kuambia wakazi wa Mlima Kenya kupitia washirika wake kwamba akimrithi hataikamilisha au kulinda maslahi yao,” asema mdadisi wa siasa Ibrahim Kamau.

DHARAU

Bw Kamau anasema katika kampeni yake ya chini ya maji, Rais Kenyatta anamsawiri Dkt Ruto kama mtu mwenye dharau anayepuuza viongozi mashuhuri wa jamii na kuchochea wakazi dhidi yao.

Dkt Ruto amekuwa akidai kwamba anachojali ni kuinua maisha ya wakazi na sio kuzungumza na viongozi kuhusu nyadhifa serikalini.

“Katika mbinu zake, Rais Kenyatta na washirika wake wanaeleza wakazi kuwa Dkt Ruto ni mwongo kwa vile hawezi kuwasaidia bila kuwa na viongozi wa kushikilia nyadhifa za juu serikalini kutoka eneo la Mlima Kenya.

Hii imeanza na kauli za Rais kuwa naibu wake alimhujumu katika kipindi chake cha kwanza uongozini hadi aliposalimiana na Bw Odinga nchi ikatulia na akaweza kufanikisha mengi,” aeleza Karanja.

Wadadisi wanasema alichofanya Rais ni kumuacha Dkt Ruto kujipiga kifua kwanza kabla ya kuanza kuchomoa silaha zake zinazoonekana kufaulu.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Geff Kamwanah, mikakati ya Rais ya kumwangamiza Dkt Ruto ilianza kubainika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi alipokutanisha viongozi wa upinzani kuwarai wamuunge Bw Odinga.

“Kwa muda wote tangu 2018, Rais Kenyatta amekuwa akisuka mipango ya urithi wake kwa msingi mmoja tu wa kuacha nchi ikiwa imeungana. Hata hivyo, kuasi kwa Dkt Ruto hasa kwa kupinga mchakato wa mageuzi ya katiba kulimfungua macho zaidi na ndio sababu anampiga vita kwa kudai anagawanya Wakenya,” asema.

Rais Kenyatta na washirika wake wa kisiasa wamenukuliwa mara kadhaa akisema kuwa hataachia nchi mtu asiyeweza kuunganisha Wakenya.

Kulingana na Bw Kamwanah, mikakati mingine ambayo Rais Kenyatta amekuwa akisuka ni kupitia mabwenyenye, wazee na watu mashuhuri kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wana ushawishi mkubwa mashinani.

Mnamo Jumanne wiki hii, mabwenyenye hao waliokutana na Bw Odinga katika hoteli ya Safari Park, Nairobi walifichua kuwa wamekuwa wakizungumza na Rais Kenyatta kuhusu siasa za urithi wake.

Naibu mwenyekiti wa wakfu wa Mlima Kenya, Bw Titus Ibui alisema kuwa Rais Kenyatta aliwataka wamshauri kuhusu siasa za urithi na wakaweka wazi kuwa wangetaka mtu atakayejali na kulinda maslahi ya eneo lao, kukamilisha miradi ya maendeleo na kuunganisha nchi.

Bw Kamau anasema kauli za waliozungumza katika hafla ya mabwanyenye hao na Bw Odinga yaliwakilisha msimamo wa Rais Kenyatta.

Duru zinasema kuwa moja ya silaha kali ambayo Rais Kenyatta ameficha ni kuunganisha vigogo wa kisiasa walio na ushawishi maeneo tofauti nchini kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Rais Kenyatta amewalenga viongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC), Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu.

Mnamo Alhamisi, wanasiasa hao walihudhuria kongamano kuu la kitaifa la wajumbe wa chama cha Kanu ambalo mgeni wa heshima alikuwa ni Bw Odinga.

“Juhudi za kuunganisha vinara wa vyama vya kisiasa chini ya Bw Odinga hazijakoma. Zinaendelea chini ya maji japo kila mmoja anaonekana kujipanga kivyake. Rais hajachoka kuwasihi kuungana ili kumshinda Dkt Ruto,” asema mbunge mmoja mshirika wa Rais Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

PANDORA PAPERS: Marais wanavyokwepa ushuru na kuficha...

Bayern Munich wapigwa ligini kwa mara kwanza katika uwanja...