Michezo

NJE TENA: Xhaka kukosa gozi la Arsenal dhidi ya Wolves

November 2nd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

HATA baada ya kupewa mwanasaikolojia baada ya tukio la kuzomewa na mashabiki kwenye mechi ya wikendi dhidi ya Crystal Palace, nahodha Granit Xhaka wa Arsenal ametemwa tena na hatakuwa kikosini kucheza dhidi ya Wolves.

Kadhalika, presha nyingi kutoka kwa mashabiki imemfanya kocha Unai Emery wa kikosi hicho kumpa nafasi kiungo mshambuliaji Mesut Ozil ambaye alionyesha kiwango cha juu dhidi ya Liverpool katika pambano la Carabao Cup.

Kwa upande mwingine, Wolves itamkosa beki matata Willy Boly aliyefanyiwa upasuaji majuzi.

Lakini huenda kocha wa kikosi hicho, Nuno Espirito Santo akarejesha uwanjani kikosi kilichovaana na Newcastle wikendi iliyopita, baada ya kufanya mabadiliko 11 Jumatano wakicheza Carabao Cup.

Wolves ambao msimu uliopita walikuwa moto wa kuotea mbali wamekuwa wakiandikisha matokeo ya kuchanganya lakini wamesonga kutoka nafasi ya 19 hadi ya 12 jedwalini.

Lakini mechi ya leo inatarajiwa kuwa ngumu baada ya timu hizo kutoka sare zilipokutana kwa mara ya mwisho mwezi Novemba.

Arsenal wamekuwa na matatizo lakini ina rekodi nzuri katika mechi za nyumbani. Wana shida kwenye safu yao ya ulinzi lakini huenda wakacheza vizuri mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Wolves iliandikisha ushindi wa 3-1 mwezi Aprili. Arsenal haijashindwa nyumbani msimu huu katika mechi nane za ligi kuu na mashindano mengine, ikijivunia ushindi mara sita.

Hawajafungwa bao katika mechi saba za nyumbani na huenda mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang akaongeza idadi ya mabao yake leo Jumamosi.

Wakati huo huo, kocha Unai Emery amesema anaungwa mkono na mtoto wa mmiliki wa klabu hiyo, Josh Kroenke, licha ya timu hiyo kuandikisha matokeo mabaya. Kroenke alikuwepo uwanjani wikendi iliyopita wakati Arsenal walitoka sare 2-2 na Crystala Palace.

“Mimi na wachezaji tunawajibika kuhusu hali ya sasa, makosa ni yetu wote na tunapaswa kujirekebisha. Nimeongea pia na mmiliki wa klabu, na akanihakikishia kwamba yupo na sisi na tayari kutoa msaada wowote,” alisema Emery.

“Nina imani na nahodha Grant Xhaka, licha ya kuzomewa na mashabiki tukicheza na Crystal Palace,” alisema kocha huyo ambaye anazongwa na uvumi kwamba huenda akatimuliwa.