Michezo

Njenga na Njeri mabingwa wa mbio za Kiambu

June 9th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MICHAEL Njenga na Lydia Njeri walitawazwa mabingwa wapya katika riadha za kilomita kumi za Henry Wanyoike Hope for the Future Run makala ya 13, kitengo cha wanaume na wanawake mtawalia zilizoandaliwa Kikuyu, Kaunti ya Kiambu.

Michael Njenga alitwaa ubingwa huo alipokamilisha mbio hizo kwa kutimka muda wa dakika 25:02 mbele ya Vincent Boit na Dancun Manyara waliokimbia kwa muda wa dakika 25:22 na 26:09 mtawalia.

“Kusema ukweli nina furaha kufuatia ushindi wangu leo. Nimekuwa nikishiriki mazoezi magumu kujiandalia mbio hizi pia hali ya hewa ilikuwa nzuri maana ilikuwa kijibaridi kiasi,” Michael Njenga alisema muda mfupi baada ya kuibuka bingwa wa mbio hizo kitengo cha wanaume.

Maureen Wambui alikimaliza wa pili kitengo cha wanawake katika mbio za Henry Wanyoike Hope for the Future Run zilizoandaliwa Kikuyu Kaunti ya Kiambu. Picha/ John Kimwere

Upande wa wanawakew, Lydia Njeri aliyekuwa akishiriki shindano hilo kwa mara ya pili alimaliza wa kwanza alipotimka muda wa dakika 30:31. Naye Maureen Wambui na Esther Waweru walitwaa nafasi ya pili na tatu walipokimbia kwa dakika 30:37 na 31:18 mtawalia.

”Hakika nashukuru sana kuibuka mshindi maana haikuwa mteremko upinzani ulikuwa mkali lakini nilifanikiwa kujikaza na kumaliza wa kwanza. Kwa sasa nalenga kuzifanyia kazi mbio za kimataifa,” Lydia Njeri alisema.

Michael Njenga na Lydia Njeri kila mmoja alituzwa Sh15,000 huku nafasi ya pili tatu kwa wanaume na wanawakew kila mmoja alipokea Sh10,000 na Sh8,000 mtawalia.

Michael Njenga akikaribia kukata utepe. Picha/ John Kimwere

Kitengo cha wanaume riadha za kilomita tisa, Ephantus Githau aliibuka mshindi baada ya kutimka dakika 27:37. Alifuatiwa kwa karibu na Simon Kimor (29:31) na Mathew Ng’ang’a (29:38).

Ubingwa wa taji hilo kitengo cha wanawake ulimwendea Lucy Wanjiku aliyetimka dakika (38:13), nao Joyce Wawera (41:11) na Hannah Muthoni (42:25) walimaliza nafasi ya pili na tatu mtawalia.