NA WANDERI KAMAU
SERIKALI imepunguza bajeti ya Hazina ya Hasla kwa Sh40 bilioni ikilinganishwa na pesa ambazo hazina hiyo ilikuwa imepangiwa kutengewa kuanzia Julai 2023.
Wadadisi wanasema hatua hiyo inaonyesha kuwa serikali itahitaji ushiriki mkubwa wa sekta ya kibinafsi ili kufanikisha mpango huo.
Kulingana na Idara ya Biashara za Kadri na Ndogo Ndogo (MSMEs), hazina hio itatengewa Sh10 bilioni katika mwaka huu wa kifedha ikilinganishwa na Sh50 bilioni ambazo serikali ilikuwa imeahidi kuitengea kwa mwaka.
Kwenye kampeni zake, Rais William Ruto aliahidi kwamba serikali ingetenga Sh50 bilioni kila mwaka kuendesha mpango huo, hilo likimaanisha kuwa serikali ingetumia hadi Sh250 bilioni kati ya 2023 na 2027.
Bunge la Kitaifa linatarajiwa kupitisha makadirio hayo mapya.
Mapunguzo hayo ya bajeti yanalingana na ahadi ambayo Waziri wa Fedha, Prof Njuguna Ndung’u, alitoa kwa Shirika la Fedha Duniani (IMF) mwishoni mwa mwaka 2022 kuwa hazina hiyo itakuwa na “ushiriki mkubwa wa sekta ya kibinafsi.”
Hazina hiyo ni miongoni mwa mikakati ya kiuchumi ambayo Rais Ruto aliahidi kuchukua ili kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira nchini, hasa miongoni mwa vijana.
Kupitia hazina hiyo, ambayo awamu yake ya kwanza ilizinduliwa Novemba 30 mwaka uliopita, Rais aliahidi kutenga mabilioni ya fedha ambayo yatatolewa kama mikopo midogo kuwasaidia wafanyabiashara wa kiwango cha chini kama wahudumu wa bodaboda.
Kufikia sasa, Wakenya wamechukua mikopo ya jumla ya Sh17 bilioni tangu kuzinduliwa kwake.
Hata hivyo, Wakenya 800,000 wamekosa kulipa mikopo hiyo kwa muda wa siku 14 ambazo zimewekwa.
kwa malipo ya mikopo iliyo kati ya Sh500 na Sh50,000. Mikopo hiyo inatozwa riba ya asilimia nane kwa mwaka.
Serikali inapanga kuzindua awamu ya pili ya hazina hiyo mwezi ujao, kwa kuongeza kiwango cha mkopo ambao mtu anaweza kuchukua kwa hadi Sh2.5 milioni.
Hatua hiyo itahakikisha kuwa kando na watu binafsi, vyama vya mashirika vitaanza kupata mikopo hiyo.