NJENJE: Matumizi ya pesa kwa njia ya simu yaongezeka

NJENJE: Matumizi ya pesa kwa njia ya simu yaongezeka

Na WANDERI KAMAU

UTUMAJI wa pesa kwa njia ya simu uliongezeka zaidi mwaka huu ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hali inayoonyesha dalili za kufufuka kwa uchumi nchini.

Kulingana na takwimu kutoka Benki Kuu ya Kenya (CBK), wahudumu wa M-Pesa (Safaricom), Airtel Money (Airtel) na T-Kash (Telkom), walipokea jumla ya Sh5.7 trilioni kati ya Januari na Oktoba mwaka huu 2021.

Fedha hizo ni ongezeko la asilimia 38, ikilinganishwa na muda uo huo mwaka 2020.

Kiwango hicho ndicho kiliongezeka kwa kasi zaidi kupokewa na wahudumu hao tangu mwaka 2011.

Mwaka huo, wahudumu hao walipokea jumla ya Sh938 bilioni.

Wadadisi wanasema huenda hali hiyo ikaendelea kushuhudiwa mwezi huu, ikizingatiwa tunaelekea katika msimu wa sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya.

Kwa kawaida, watu wengi hutumia pesa kwa wingi msimu huo kutembelea jamaa zao katika maeneo ya mashambani au kutembeza familia zao katika maeneo tofauti nchini.

Ongezeko hilo linaonyesha dalili za kufufuka kwa uchumi, hasa katika sekta za uchukuzi, elimu, habari, mawasiliano na biashara ndogo ndogo.

Katika robo ya pili ya mwaka, uchumi wa nchi ulikua kwa asilimia 10.1, kiwango hicho kikiwa cha juu zaidi katika miongo minne iliyopita.

“Dalili zinaonyesha uchumi unaendelea kuinuka, hasa katika sekta zilizoathirika sana kutokana na janga la virusi vya corona. Ukuaji huo umechangiwa pakubwa na serikali kuifungua nchi,” akasema Gavana wa CBK, Dkt Patrick Njoroge.

Wakenya pia walikumbatia pakubwa utumaji pesa kwa simu kutokana na tahadhari zilizotolewa na serikali mwaka 2020 ili kudhibiti maambukizi ya corona.

Matumizi ya noti na sarafu yalionekana kama njia moja ya kueneza virusi hivyo hatari.

Ukumbatiaji huo vile vile ulichangiwa na hatua ya kampuni za simu kuondoa ada za kutuma pesa chini ya Sh1,000.

Idadi ya wahudumu hao iliongezeka kutoka 287,410 mnamo Januari hadi 295,105 kufikia Oktoba.Nayo idadi ya watumizi wa huduma hizo iliongezeka kutoka 66.6 milioni hadi 66.9 milioni katika muda huo.

You can share this post!

ZARAA: Siri ni kukuza pilipili mboga za rangi tofauti...

Museveni atuma jeshi kumzima Bobi Wine

T L