NJENJE: Pakistan sasa yaongoza kwa ununuzi wa bidhaa za Kenya

NJENJE: Pakistan sasa yaongoza kwa ununuzi wa bidhaa za Kenya

NA WANDERI KAMAU

PAKISTAN iliipita Uganda kama nchi ambayo Kenya inauza bidhaa zake kwa wingi, kwenye robo ya kwanza ya mwaka huu, kulingana na takwimu ambazo zimetolewa na Shirika la Kitaifa la Kukusanya Takwimu (KNBS).

Hali hiyo imechangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya majanchai.

Mauzo ya Kenya nchini Pakistan yaliongezeka kwa asilimia 21.5; yakifikia Sh16.9 bilioni ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka uliopita, ambapo yalifikia Sh13.9 bilioni.

Mauzo ya bidhaa nchini Uganda yaliongezeka kwa asilimia 0.4 mwaka huu, kwa kufikia Sh16.7 bilioni.

Pakistan ndilo taifa linalonunua majanichai ya Kenya kwa wingi zaidi ikilinganishwa na nchi nyingine.

Mauzo ya zao hilo yaliongezeka sana, baada ya taifa hilo kuondoa ada ya asilimia 0.5 iliyokuwa ikitoza majanichai yaliyokuwa yakiingizwa huko kutoka nchi za nje.

Kwa muda mrefu, wadau katika sekta ya majanichai wamekuwa wakiishinikiza Pakistan kuondoa ada hiyo, wakisema ilikuwa ikichangia majanichai ya Kenya nchini humo kuwa ghali ikilinganishwa na mataifa mengine.

Nchi nyingine zilizonunua bidhaa za Kenya kwa wingi ni Uholanzi na Amerika. Mataifa hayo yalinunua bidhaa za thamani ya Sh15.9 bilioni na Sh14.8 bilioni mtawalia.

Hata hivyo, pengo kati ya bidhaa ambazo Kenya iliuza na ilizoagiza kutoka nchi za kigeni liliongezeka kwa asilimia 10.8 (au Sh34.2 bilioni).

Hilo limetajwa kuchangiwa na kuongezeka kwa bei za mafuta na bidhaa nyingine kama ngano.

Kenya iliagiza bidhaa za thamani ya Sh591.6 bilioni ikilinganishwa na mauzo yake ya Sh351.6 bilioni katika nchi za kigeni.

Hilo ni licha ya kuongezeka kwa mauzo ya Kenya hadi Sh240.1 bilioni.Wadadisi wanasema takwimu hizo zinaonyesha kuwa uchumi wa Kenya unaendelea kukua.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Wakulima washauriwa wafanye vipimo vya udongo

CECIL ODONGO: Ruto achunge ulimi wake, sifa ya ukabila...

T L